Nyota wa muziki wa kizazi kipya Afrika, Nasibu Abdul maarufu Diamond Platnumz ameingia kwenye vita ya kupambano kwa kuwataka vijana nchini, kuachana matumizi ya dawa za kulevya kwani hazina manufaa yoyote katika maisha yao.
Diamond amezungumza hayo katika maadhimisho ya kitaifa ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya katika Uwanja wa Sheikh Amri AbeidĀ leo Jumapili, Juni 25, 2023 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema matumizi ya dawa za kulevya licha ya kuharibu afya pia uvutaji unaondoka fursa kwa vijana.
“Ukiwa unatumia dawa za kulevya unaitwa teja hakuna ambaye atakupa kazi, hakuna ambaye atakupokea hata katika muziki sisi tukikuona tunakuona teja tu,” amesema.
Amesema hakuna faida yoyote katika dawa za kulevya na matumizi yake yanaondoa ndoto za kuishi vizuri wala kuaminiwa katika jamii ikiwepo kupata kazi.
“Leo mimi nimetoka Tandale nimefika Arusha kwa sababu naaminiwa,” amesema Diamond.
Ujumbe huo wa Diamond ambaye pia ni Mkurugenzi wa Wasafi Media, ulishangiliwa na mamia ya watu ambao wanashiriki katika maadhimisho hayo.