Waziri Mkuu mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, John Malecela ametoa kauli kuhusu sakata la makubaliano ya uwekezaji wa bandari nchini na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni ya Dubai Port World (DPW).
Malecela ametoa kauli hiyo leo Jumapili Juni 25, 2023 baada ya kuulizwa swali kuhusiana na uwekezaji huo unaohusisha Serikali hizo mbili.
Malecela amesema haoni shida ya uwekezaji huo na amewashangaa wanaopinga akisema ndio demokrasia inavyowaruhusu.
“Kwanza wako wachache wanaopinga na sioni hoja yao,” amesema Malecela ambaye ni Waziri Mkuu wa saba wa Tanzania akipokea nafasi hiyo kutoka kwa Jaji Joseph Warioba.
Leo, Malecela amekutana na waandishi wa habari nyumbani kwake eneo la Kilimani jijini Dodoma akielezea kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Malecela alikuwa Waziri kuanzia Novemba 9, 1990 hadi Desemba 5, 1994 na nafasi yake kuchukuliwa na Fredereck Sumaye.
Amewataka Watanzania kumuunga mkono Rais Samia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Malecela pia amekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (2005-2009), Balozi wa Tanzania nchini Uingereza (1989-1999), Waziri wa Utamaduni Chakula na Usalama (1975-1980), na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (1972-1975).