Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameonya gereji zinazofanya biashara ya unga unaotoka katika masega ya gari kwa ajili ya kutengenezea dawa za kulevya.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumapili Juni 25, 2023 katika maadhimisho ya kitaifa ya kupiga vita matumizi na biashara ya dawa hizo duniani ambayo kitaifa yamefanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
“Wanachukua huo unga kwenye magari wanakwenda kuchanganya na dawa za kulevya na ndio sababu watumiaji wa dawa hizo wanafariki ghafla,”amesema Rais Samia.
Pia, Rais Samia amesema amewataka wamiliki wa gereji za magari na vyombo vya dola vinapaswa kushughulikia jambo hilo.
Hata hivyo, amesema Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inafanya kazi nzuri Kudhibiti dawa ambazo zinatumika kuchanganywa na dawa za kulevya.
Akizungumzia kauli hiyo ya Rais Samia, Jeremia Msangi mkazi wa Jiji la Arusha ameunga mkono hoja ya Rais huku akitoa ushuhuda namna gari lake lilivyotolewa masega.
“Mimi walikata kabisa Exosti yangu na kutoa unga huo (masega) na kuichoma sijui ni gereji ipi ila hili tatizo ni kubwa na aliyebaini ni fundi wangu mwingine baada ya gari kukosa nguvu,”amesema.