MARA baada ya kutangazwa rasmi kuwa kocha mkuu mpya wa Yanga, Miguel Gamondi raia wa Argentina amekabidhiwa rasmi ripoti ya maboresho ya kikosi hicho iliyoachwa na Kocha Nasreddine Nabi kwa ajili kutoa msimamo wake, huku mwenyewe akichimba mkwara kwa mastaa wote akiwemo Fiston Mayele kwa kusema anataka kutengeneza timu ya makombe.
Gamondi alitangazwa rasmi kuwa kocha mkuu wa Yanga juzi Jumamosi kupitia mkutano mkuu wa Yanga ambao ulifanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere akichukua nafasi ya aliyekuwa Kocha wa Yanga Mtunisia, Nasreddine Nabi.
Chanzo chetu cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Championi Jumatatu, tayari uongozi wa Yanga chini ya Injinia Hersi umekabidhi ripoti ya maboresho ya kukosi kwa kocha huyo.
“Mara baada ya kumtangaza kocha mkuu mpya wetu, bila kupoteza muda uongozi umemkabidhi faili la wachezaji wote ili kufanya mapitio na kutoa msimamo wake wa mwisho, unajua shughuli zote za usajili zilisimama kwa muda kupisha mchakato wa kumtangaza kocha mpya sasa kila kitu kinasubiri tamko lake.” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza namna anavyotaka kusuka kikosi chake Gamondi alisema: “Nafahamu Yanga ni timu kubwa Tanzania na Afrika Mashariki, msimu uliopita ulikuwa wa mafanikio makubwa kwao nami naamini kama wote tutakuwa na nidhamu, ushirikiano na kupambana kama timu basi tutajenga kikosi imara na kushinda tena makombe.”
AANZA NA NYUNDO TANO
Katika hatua nyingine Championi Jumatatu limefanya tathmini na kugundua kocha huyo atakuwa na nyundo tano ambazo anatakiwa kuanza nayo ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao.
Miongoni mwa nyundo ambazo kocha huyo atakumbana nazo akiwa kwenye jezi hizo za Yanga ni pamoja na kupitia njia ya kocha aliyepita, Nasreddine Nabi ya kubeba mataji yote ya ndani na kuzima utawala wa wapinzani wao Simba.