Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo ameigiza kuanza kufanya kazi kwa kituo cha afya cha Mbutu, ili kurahisisha huduma za matibabu kwa wakazi wa Kata ya Somangila.
Bulembo ametoa agizo hilo jana Jumatatu Juni 26, 2023 katika mwendelezo wa ziara yake ya mtaa kwa mtaa akiwa katika kata ya Somangila wilayani Kigamboni.
“Nimefika Somangila, nimekuta kituo cha hiki kilichongejengwa Mtaa wa Kichangani kwa fedha za tozo bado hakijaanza kufanya kazi. Nimemuelekeza mganga mkuu wa wilaya kuhakikisha kinaaza kazi mara moja.
“DMO (Mganga mkuu wa wilaya) amenihakikishia kuanzia Julai Mosi kitaanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje, lakini ikifika Oktoba huduma zote zenye hadhi ya kituo cha afya,” amesema Bulembo.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kigamboni, Lucas David amesema maandalizi kwa ajili ya kuanza kazi kituo hicho, yamekamilika ikiwemo kupokea watumishi, sambamba na vifaa tiba.
“Tutaanza na huduma kwa wagonjwa wa nje na maabara, kwa hiyo kuanza sasa wananchi wajiandae na matunda ya uwepo wa kituo hiki,” amesema Dk David.
Akizungumza na Mwananchi katika ziara hiyo, Mkazi wa Mbutu, Rachel John amesema kina mama ndio waathirika wakubwa kupata huduma za matibabu akisema kwa sasa hospitali zipo mbali na eneo hilo.
“Kwa mfano nina ujauzito ninahitaji kufika hospitalini kwa muda mwafaka, najikuta nashindwa kwa sababu ya changamoto ya usafiri. Unajikuta usiku unatafuta bajaji ikufikishe kituo cha afya, lakini hiki kikianza kitakuwa na ahueni,” amesema Rachel.
Katika hatua nyingine, Bulembo aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Kagera, amewataka wanaoyamiliki mapori katika kata hiyo kuyaendeleza.
“Tangu naanza ziara hii katika kata zingine nimekuwa nikisitiza jambo hili, wasipoyaendeleza kwa mujibu wa sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 inaturuhusu kuwanya’nganya.
“Wenye hati zao ambazo wamekaa kwa miaka mitatu bila kuyaendeleza, wanatakiwa kuwanyang’anya. Narudi wenye maeneo Kigamboni yaendelezeni kabla ya Serikali haijachukua hatua ya kuyarejesha,”amesema Bulembo.