Na Evelyne Ernest – Kagera
Watoto wawili wa familia moja wamekutwa wamefariki baada ya kufukiwa na mawe wakati wakichimba mchanga katika eneo la Maharahara Kijiji cha Magata Kata ya magata Karutanga Wilayani Muleba Mkoani Kagera.
Diwani wa kata ya Magata Karutanga Alhaji Yakubu Mahamudu amesema kuwa watoto hao walikuwa wanachimba mchanga ndipo hapo jana wakaweza kufukiwa na mawe ambapo leo hii wameweza kuokolewa na jeshi la zima moto kwa kushirikiana na wananchi.
Alhaji Yakubu amewataja watoto hao ni Samsoni Eliudi mwenye umri wa miaka 13 na Emmanuel Eliud mwenye umri wa miaka 10 ambapo wote walikuwa wanafunzi wa shule ya Msingi Magata huku chanzo cha watoto hao kujihusisha na uchimbaji wa mchanga ni baada ya kutelekezwa na baba yao mazazi na kubaki na mama yao pekee.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga amepiga marufuku eneo hilo kutotumika kwa shughuli zozote za uchimbaji wa mchanga kutokana na mazingira hayo sio rafiki huku akiagiza viongozi wa vijiji na kata kukagua maeneo yote ya uchimbaji wa mchanga katika Wilaya hiyo ili kudhibiti maafa yasiweze kuendelea kutokea.
Nao baadhi ya wananchi ambao ni Ashimu Salimu na Godfrey Joel wamesema kuwa tukio hilo limewasikitisha huku wakiomba kudhibiti vitendo vya baadhi ya wazazi kutelekeza watoto watoto wao.
Aidha jeshi la Polisi Wilayani Muleba limefika eneo la tukio na kuruhusu taratibu za mazishi ziendelee.