MARA baada ya jana Jumatano kutangaza rasmi kuwa tayari mzigo wa jezi zao mpya kwa msimu wa 2023/24 umefika, uongozi wa Simba kupitia kwa Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally amechimba mkwara mzito kuwa jezi hizo zitavunja rekodi ya mauzo kutokana na ubora mkubwa ilizonazo.
Kwa mara ya kwanza msimu huu tenda ya usambazaji wa jezi za Simba itafanywa na Kampuni ya Sandaland mara baada ya kushinda tenda ya miaka miwili kupitia mkataba ambao uliingiwa Juni 16, mwaka huu.
Kampuni ya Sandaland imetangaza kuwa tayari mzigo wa jezi mpya za msimu wa 2023/24 umewasili Tanzania na unatarajiwa kuuzwa mara tu baada ya kutambulishwa rasmi mwanzoni mwa mwezi Julai.
Akizungumza , Ally alisema: “Tayari jezi zetu mpya kwa msimu ujao wa 2023/24 umewasili kwa idadi ya kutosha kwa kila Mwanasimba kupata jezi yake ambapo tunatarajia kufanya uzinduzi wa jezi hizo mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
“Kama uongozi tunachoweza kuwahakikishia Wanasimba ni kuwa ubora wa jezi hizi haujawahi kutokea tangu biashara ya jezi imeanza kufanyika na tunakwenda kuvunja rekodi ya mauzo, hivyo Wanasimba wakae tayari.”