Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Khadija Shaaban Taya (Keisha) amewaomba watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo na kutoa ufafanuzi kuhusu Suala la Bandari ya Dar es salaam kwani linakwenda kugusa maisha ya watanzania.
Keisha amewataka watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ambazo Serikali inazitengeneza ikiwemo fursa za ajira zinazotangazwa.
Amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuwainua wananchi kiuchumi, kukuza ujuzi lakini mwamko wa watu wenye ulemavu kushiriki katika fursa hizo umekuwa mdogo sana.
Ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati wa hafla ya chakula cha mchana na watu wenye ulemavu iliyoandaliwa yeye mwenyewe iliyofanyika katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Dodoma.
Kuhusu sakata la bandari kuendeshwa na DP WORLD, Mbunge Keisha amewataka watu wenye ulemavu nchini kuacha kutishwa na kuogopa maneno yanayoongelewa mtaani juu ya makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari nchini namatokeo yake wachangamkie fursa hiyo ili kuweza kujikwamua kiuchumi.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo ya chakula cha Mchana na watu wenye ulemavu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Kazi, Vijana na watu wenye Ulemavu) Mhe Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka fursa mbalimbali kwaajili ya watu wenye ulemavu ikiwemo kuwawezesha kufanya ujuzi na bunifu kwa kuwajengea Vyuo vya Ufundi.
Mhe Ndalichako amesema kuwa Serikali imetenga jumla tsh. Bilioni tatu kwaajili ya ujenzi wa vyuo vya watu wenye ulemavu hiyo ni kwa ajili ya kuendeleza vyuo hivyo.
Prof. Ndalichako amesema mpaka sasa wanajenga vyuo vipya vitatu vya watu wenye ulemavu kwa mikoa mitatu ikiwemo Kigoma, Songwe na Ruvuma na kuwataka kuchangamkia fursa zinazotolewa kwenye mikopo yao.