Dereva wa bodaboda Kahii Ga Cucu wa Kaunti ya Kiambu nchini Kenya, ameelezea furaha yake baada ya kufanikiwa kujenga nyumba yenye thamani ya Sh17,300,000 ya fedha ya Kitanzania.
Kijana huyo mwenye miaka 35, amesema anajivunia kumiliki nyumba nzuri ambayo imemgharimu zaidi ya Sh1 milioni ya Kenya.
Ga Cucu amesema alianza kujenga nyumba hiyo baada ya kuajiriwa kama dereva bodaboda na kilichomsukuma ni kutokana na changamoto za maisha zilizomsababishia kuacha masomo ya chuo kikuu.
Kupitia mtandao wa TUKO, kijana huyo amesema amefanikiwa kuimalizia nyumba yake ndani na nje kisha kuweka samani mbalimbali muhimu zinazohitaji.
“Nimeweka TV kubwa, viti vya kupendeza na meza ya kuvutia, amedokeza kijana huyo.
Amesema alilelewa katika mazingira ya magumu, kwani wazazi wake walipofariki, yeye na ndugu yake mmoja waliachwa wakilelewa na bibi yao, ambaye naye alifariki wakati yeye akiwa chuoni.
Kijana huyo ameelezea kuwa muda mfupi baada ya kifo cha bibi yake, alikumbana na changamoto za kifedha na kulazimika kuacha masomo.
“Nikaamua kufanya kazi kama dereva wa bodaboda kwa sababu nililazimika kumlea mdogo wangu. Baadaye nilimudu kununua pikipiki yangu mwenyewe,” amesema.
Anasema shida alizopitia zilimjenga na kumfanya kuwa na shauku ya kumiliki nyumba yake mwenyewe.
“Nimejenga nyumba tayari, pia nilitumia zaidi ya milioni moja kwa sababu ina muundo maalumu, kama unavyoona (pichani). Pia niliweka samani na vifaa vyenye ubora ili nipate faraja niliyoitamani,” amesema.
Kahii amefanikiwa kununua bodaboda tatu ambazo amewaajiri wenzake katika kazi hiyo.