Ilikuwa mshtuko baada ya ndugu wa marehemu Steven Hamis Massawe (60) kufika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi na kuukosa mwili wa ndugu yao.
Tukio hilo lilitokea juzi, baada ya ndugu hao kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kuuandaa mwili kwa maziko yaliyotarajiwa kufanyika jana, lakini kumbe mwili wa ndugu yao ulishachukuliwa tangu Juni 26 na kuzikwa siku hiyo hiyo Chalinze, mkoani Pwani kwa imani ya Kiislamu.
Tukio hilo ni miongoni mwa matukio kadhaa ya kubadilisha miili ya marehemu yaliyotokea hivi karibuni, likiwamo la mkoani Mbeya ambako mwili wa mwanajeshi mstaafu, Watson Mwambungu ulikwenda kuzikwa Wilaya ya Busokelo baada ya kuchukuliwa na watu wengine Juni 15.
Tukio lingine lilitokea Mei 19 baada ya ndugu wa marehemu Melkior Ndambale kwenda mahakamani kuomba kibali cha kufukua mwili wa ndugu yao uliokuwa umezikwa kimakosa wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro.
Katika tukio la sasa, marehemu Steven Massawe, aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji cha Omarini Kibosho, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro alifariki Juni 24, mwaka huu nyumbani kwake na mwili kupelekwa kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya Mawenzi.
Hata hivyo, Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Edna-Joy Munisi alipotafutwa kwa simu kuzungumzia tukio hilo, simu yake iliita bila kupokewa.
Jana, ndugu wa marehemu, Thobias Massawe alisema Juni 28, mdogo wa marehemu alikwenda Hospitali ya Mawenzi kwa ajili ya kuhakiki mwili, lakini hakuukuta katika chumba cha kuhifadhia maiti, jambo lililoibua mshtuko.
“Mazishi yalikuwa yafanyike leo (jana) Alhamisi, lakini hakuuona mwili na baada ya kuutafuta bila mafanikio, alitoa taarifa kwa uongozi wa hospitali ambao walifanya ukaguzi na kujiridhisha mwili haupo.
“Walianza kufanya ufuatiliaji kujua mwili umechukuliwa na nani na ndipo walipobaini kumefanyika makosa, kwani marehemu mwingine anayeitwa Idd mwili wake umebaki mochwari na ndugu walichukua mwili wa Steven na kwenda kuuzika Chalinze,” alisema.
Alisema ndugu wa Idd walichukua mwili tangu Jumatatu Juni 26 na pia ni Waislamu.
“Walikwenda kuuzika Jumatatu Chalinze na walizika kwa imani ya dini ya Kiislamu, huu uliobaki hapa si wetu, hivyo baada ya kugundua hivyo zikafanyika taratibu zikiwemo za kisheria kupata vibali, ili kwenda kuufukua mwili Chalinze,” alisema.
Alisema kwa kushirikiana na uongozi wa hospitali, walichukua mwili wa Idd ulioachwa Mochwari wakaenda nao, ili kufanya taratibu za kuufukua mwili wa Massawe na kuurudisha Kibosho Mkombole Kilimanjaro kwa ajili ya maziko.
Aidha, alisema kwa sasa taratibu nyingine zinaendelea nyumbani kwa marehemu wakati wakiendelea kusubiri mwili wa marehemu, ili kuona kama utawahi kufika na kuuzika.
“Tukio hili limetusababishia hasara na usumbufu mkubwa, maana mpaka sasa hatujui kama tutawahi kuuzika leo licha ya kwamba maandalizi ya vyakula, vinywaji viliandaliwa na hata MC ameshalipwa na waombolezaji wamekaa kusubiri maziko ya mpendwa wetu,” alisema.
Raymond Massawe ambaye ni kaka wa marehemu, alisema tukio hilo limeonyesha hakuna umakini katika eneo hilo na kuiomba Serikali kuwawajibisha wale ambao wamehusika na uzembe huo.
“Uzembe uliofanyika hapa Hospitali ya Mawenzi ni mkubwa na inaonekana hawako makini, kama mwili wa mtu utaletwa hapa, halafu ubadilishwe apewe mtu mwingine, wanaweza pia kubadilisha wa mtoto na kuchukua mtu mzima,” alisema Massawe.