Rais mteule wa Liberia, Joseph Boakai, ambaye ameshinda rais George Weah, katika duru ya pili ya urais wa Novemba 14, anasema utawala wake utaangalia kwa karibu mikataba ya uchimbaji madini ili kuhakikisha kuwa inanufaisha nchi.
Amesema kinachofuata ni kushughulikia masuala ambayo yanarudisha nyuma nchi na kutaja ufisadi na ukosefu wa huduma za msingi.
Boakai amesema eneo muhimu ambalo Waliberia hawajanufaika nalo ni sekta ya madini, licha ya kuwa na akiba kubwa ya madini katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, ikiwa ni pamoja na almasi, dhahabu, madini ya chuma na mbao.
Nimeona rasilimali zetu zikinyonywa na maisha ya watu yanabaki kuwa mabaya zaidi, Boakai alisema,na kuongeza kuwa ataangalia kwa karibu sekta hiyo.
Alipoulizwa kama hii itajumuisha kupitia upya mikataba ya uchimbaji madini, Boakai amesema mapitio yatafuatiliwa iwapo itahitajika kufanya hivyo.