Dodoma. Serikali imesema baada ya Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kufanya uchambuzi wa madai hayo kilichokuwa kiwanda cha Nguo cha Sunguratex imeonekana kuwa wafanyakazi hao walishalipwa mafao kikamilifu.Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi leo Februari Mosi, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Ukonga (CCM), Jerry Silaa.
Slaa alitaka kufahamu ni lini Serikali itawalipa mafao waliokuwa wafanyakazi wa viwanda vya Kiltex na Sunguratex Gongolamboto.
Akijibu Katambi amesema, kuanzia mwaka 1989 Serikali kupitia mifuko ya NSSF na uliokuwa PPF iliwalipa mafao waliokuwa wafanyakazi wa viwanda vya Kiltex na Sunguratex Gongolamboto baada ya ukomo wa ajira zao.
Hata hivyo, amesema Aprili mwaka 2022 mfuko wa PSSSF ulipokea malalamiko ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda Sunguratex wapatao 644 wakidai kuwa hawakulipwa mafao yao kikamilifu na uliokuwa mfuko wa PPF.