Tazara imezindua behewa jipya lenye uwezo wa kubeba mzigo tani 200 na litabeba mitambo mikubwa inayohitajika kufua umeme wa maji kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Dar es Salaam. Katika kuongeza ufanisi wa usafirishaji mizigo shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) limezindua behawa jipya lenye uwezo wa kubeba mzigo wa tani 200 kwa wakati mmoja.
Behewa hilo lenye uzito wa tani 115 limetengenezwa nchini China huku thamani ya mradi mzima ikiwa dola 700,000 sawa na Sh2 bilioni.
Akizungumza kweye hafla ya uzinduzi wa behewa hilo leo Februari Mosi, mgeni rasmi Mkurugenzi wa huduma za Uchukuzi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Aron Kisaka amesema behewa hilo ni kubwa na halijawahi kuwepo katika nchi za Afrika.
“Kwa hiyo ni la kwanza na limejengwa maalumu Kwa ajili ya kubeba mizigo inayokwenda katika mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, ambapo baadhi ya mizigo ni mipana zaidi na mirefu ambayo mabehewa ya kawaida hayana uwezo wa kubeba,” amesema.
Amesema katika kuhakikisha mradi huo unakamilika serikali awamu ya kwanza ilitoa fedha Kwa ajili ya matengenezo ya kituo cha reli cha Fuga kitakachokuwa mahususi kwa kupokea mizigo hiyo.
“Matengenezo ya kituo hicho yalianza tangu mwaka 2018 na yamekamilika na wataalamu wetu walianza kufanya usanifu wa mabehewa yanayoweza kubeba mizigo vifaa vinavyohitaji kutumika katika bwawa la Mwalimu Nyerere,” amesema.
Amesema baada ya kumaliza usanifu wakaandaa michakato yote ikiwemo kuagizia na hatimaye wamepokea behewa hilo litakalokuwa linabeba mizigo ya vifaa hivyo.
Meneja Mkuu wa Tazara, Fuad Abdallah amesema walinunua behewa hilo baada ya serikali kuanza kutekeleza mradi wa Bwawa hivyo walilazimika kufanya hivyo kubeba mitambo itakayo hitajika ambayo inaurefu wa mita hadi saba
“Mabehewa tuliyonayo yanauwezo wa kubeba mita 2.6, kulingana na ukubwa huo wa mitambo hiyo mabehewa yetu yaliyokuwepo haikuwa na uwezo wa kubeba,” amesema.