Kamishna wa Umeme Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga ameridhishwa na hatua mbalimbali za maendeleo katika upatikanaji wa huduma ya Umeme Mkoa wa Shinyanga huku akipongeza kwa kuongeza makusanyo ya mapato kutoka bilioni 8 hadi kufikia bilioni 11 katika Mwaka huu wa fedha 2023\2024
Mhandisi Luoga ameyasema hayo leo Juni 24,2024 baada ya kufanya ziara yake ya siku moja mkoani Shinyanga ambapo ametembelea mradi wa Umeme wa Jua katika Wilaya ya Kishapu pamoja na kituo cha kupoza na kusambaza Umeme Ibadakuli.
Akisoma taarifa ya miradi ya kusambaza Umeme kwa Mwaka wa fedha 2023\2024 meneja wa shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Leo Mwakatobe amesema mradi wa Umeme wa Jua unaotekelezwa katika maeneo ya Ngunga Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga umefikia asilimia kumi (10) ambapo unatarajiwa kukamilika Mwezi Februari 2025.
Mhandisi Mwakatobe ameeleza zaidi kuwa hali ya usambazaji Umeme katika Mkoa wa Shinyanga imeendelea kuimarika ambapo jumla ya vijiji 412 kati ya vijiji 509 tayari vimefikiwa na Umeme huku akisema ipo mikakati ya kuhakikisha vijiji 97 vilivyobaki vinafikia na miundombinu ya Umeme mwishoni mwa Mwaka huu 2024.
“Hali ya usambazaji Umeme imeendelea kuimarika kutokana na miradi mbalimbali ya kusambaza Umeme inayotekelezwa na TANESCO na ile ya kusambaza Umeme vijijini inayofadhiliwa na serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA)”.
“Jumla ya vijiji 412 kati ya 509 vimefikiwa na Umeme na matarajio yetu ifikapo mwishoni mwa Mwaka 2024 vijiji vyote 97 vilivyobaki Mkoani Shinyanga vitakuwa vimefikiwa na miundombinu ya Umeme”.
“Katika Manispaa ya Kahama vijiji 37 kata ya 45 vimefikiwa na Umeme, Halmashauri ya Msalala vijiji 45 kati ya 92 vimefikiwa na Umeme, Halmashauri ya Ushetu vijiji 84 kati ya 112 vimefikiwa na Umeme, Manispaa ya Shinyanga vijiji 11 kati ya 17 vimefikiwa na Umeme, Shinyanga vijijini vijiji 121 kati ya 126 vimefikiwa na Umeme na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu vijiji 114 kati ya 117 tayari vimefikiwa na Umeme”,amesema Mhandisi Mwakatobe.
Pia meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga pamoja na mambo mengine amesema shirika hilo linasimamia miradi miwili (2) ya kimkakati ambayo ni mradi wa Umeme wa Jua Wilaya ya Kishapu pamoja na mradi wa kuboresha upatikanaji Umeme Bulyanhulu ikiwa lengo ni kuongeza uzalisha Umeme na kuboresha upatikanaji Umeme.
“Mradi wa Umeme wa Jua, kutokana na mahitaji ya Umeme kuongezeka serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Umeme Jua maeneo ya Ngunga Kishapu ili kuongeza kiwango cha upatikanaji Umeme Mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine ya Nchi, mradi huu unatarajiwa kuzalisha Umeme wa kiasi cha Megawati 150 ambapo mradi unathamani ya shilingi 323, 059,197, 768.30 na umegawanyika katika awamu mbili ya kwanza ni MW 50 na mkandarasi ni SINOHYDRO ambapo mkandarasi ameshakabidhiwa kazi na kuanza ujenzi Mwezi Oktoba 2023, kwa sasa mradi upo asilimia 10 na matarajio ya kukamilika ni baada ya Miezi kumi na nne (14).
“Mradi wa kuboresha upatikanaji Umeme uliopo eneo la Bulyanhulu, serikali kupitia shirika la Umeme kwa Mkoa wa Shinyanga kwa kuongeza mashineumba au Transfoma yenye ukumbwa wa 90\120MVA kwenye kituo cha kupoza Umeme wa grid cha Bulyanhulu 220\33kV mradi huu una thamani ya dola za kimarekani 5,318,800.00 (bilioni 12) na mradi unatarajia kukamilika Septemba 2024”,amesema Mhandisi Mwakatobe
Aidha Mhandisi Mwakatobe ametaja mafanikio mbalimbali yaliyofikia na shirika la Umeme TANESCO Mkoa wa Shinyanga katika Mwaka wa fedha 2023\2024 ikiwemo ongezeko la ukusanyaji mapato kutoka bilioni nane (8) hadi kufikia bilioni kumi na moja (11).
“Katika utekelezaji wa miradi ya kusambaza Umeme kwa Mwaka wa fedha 2023\2024 tumefanikiwa kuunganisha wateja mpaka kufikia wateja 95,206 lakini pia tumefanikiwa kuongeza mtandao wa usambazaji Umeme hadi kufikia kilomita 2,331.05 kwa msongo wa kati na kilomita 2,328.72 kwa msongo mdogo, tumefanikiwa kufikisha Umeme kwenye jumla ya vijiji 412 kati ya vijiji 509 lakini pia tumefanikiwa kuongeza makusanyo ya mapato hadi kufikia bilioni 11”,amesema Mwakatobe.
Akizungumza kamishna wa Umeme Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga amempongeza meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga na menejimenti yake kwa usimamizi mzuri wa miradi ya Umeme huku akiwasisitiza wakandarasi kukamilisha kwa wakati miradi inayoendelea ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali
“Kwanza nikupongeze meneja pamoja na menejimenti yako yote kwa usimamizi mzuri kwa sababu hali ya Umeme sasa hivi Mkoa umetulia makusanyo yameongezeka kwa sababu kipimo cha utendaji wa menejimenti moja wako ni ongezeko la mapato kwahiyo nawapongeza sana kwa kuongeza mapato kingine nawapongeza kwa kuongeza wateja hapo hapo niwasisitiza tujitahidi sana kuongeza kasi ya kuunganisha wateja wapya ili kuongeza mapato”.
“Pia tuwe na mikakati maalum ya kuhakikisha tunazuia au tunapunguza upotevu wa Umeme sasahivi tunasisitiza sana matumizi bora ya nishati safi lakini pia tuendelee kudai madeni ya taasisi zinazodaiwa na tuweke mikakati ya kukusanya madeni hayo tutumie njia ambazo zinawezekana ikiwemo kukaa vikao nao ili kuweka maazimio ya pamoja pamoja na kwa wale wateja wadogo wadogo”.