Naibu Waziri wa Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Injinia Kundo Mathew amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la Wizara hiyo chini ya Waziri Nape Moses Nnauye la kufuta tozo katika miamala ya simu.
Naibu Waziri Kundo ameyasema haya leo July 04,2023 akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Rukwa.
“Fahari ya Mh. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Rais ni pamoja na kuwasikiliza Watanzania na Wananchi anaowaongoza, ndio maana ameruhusu na kutoa maelekezo ya moja kwa moja kuondoa tozo katika miamala ya simu”
“Rais wenu kipenzi Mkuu wa Nchi ameruhusu na kutoa maelekezo tozo inayotokana na miamala ya simu iondolewe, hakutokuwa na tozo kwenye miamala ya simu, ile tozo mliokuwa mnasema Rais ameshapangua huyu ndio Mwanamapinduzi halisi wa maendeleo ya Taifa letu”
“Kila Mtu kwenye Familia yake ajue kwamba kuondoka kwa tozo hii ambayo ulitakiwa ukatwe labda Tsh.Elfu 5 haujanunua mboga jamani? ni Rais mmoja tu ambaye ameona uchungu wa Watu wake na sisi tumuunge mkono” amesema Naibu Waziri Injinia Kundo.
Tozo za miamala ya simu zimefutwa rasmi Julai Mosi baada ya kudumu kwa kipindi cha miaka miwili tangu kufanyika kwa marekebisho kwenye Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa sura 437 na Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki, sura ya 306 na kupitishwa na Bunge Mwaka wa fedha 2021/22.
Kufutwa kwa Tozo za Miamala ya Simu kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kumepokelewa kwa mitazamo tofauti na baadhi ya wadau na wamiliki wa Kampuni za Mawasiliano nchini wakisema hatua itachochea matumizi ya kielektroniki katika miamala mbalimbali.