KLABU ya Yanga imealikwa na Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya Uhuru wa Taifa hilo zitakazofanyika Julai 6, mwaka huu nchini huko.
Katika sherehe hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atahudhuria.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga , Ally Kamwe, alisema kuwa wachezaji wote waliokuwa kwenye mapumziko wamekubali kuhudhuria maadhimisho hayo na Julai 5, wataondoka na ndege maalum wakiwa na wachezaji takribani 15 kutoka kikosi kikubwa na wengine 22 kutoka Timu ya Vijana ya U20.
Kamwe alisema kuwa kesho Jumatano mara baada ya kutua Malawi, watakuwa na hafla ya chakula cha jioni Ikulu na Rais wa Malawi.
Alisema kuwa katika sherehe hizo, Yanga watapata nafasi ya kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Nyasa Big Bullets ya nchini Malawi.
“Yanga tumepata mwaliko kutoka kwa Rais wa Malawi keshokutwa (kesho) Jumatano kwa ajili ya kupata nao chakula cha jioni ambapo katika hafla hiyo walioalikwa ni wachezaji pamoja na viongozi pekee.
“Mwaliko huo ni maalumu kutoka kwa Serikali ya Malawi kucheza mchezo maalumu kwenye maadhimisho ya miaka 59 ya Uhuru, ni heshima kubwa sana kwa klabu yetu na kwa taifa kwa ujumla.
“Mgeni wa heshima kwenye Sikukuu za Uhuru wa Malawi ni Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Malawi ikatupa heshima hii ya kipekee kwa mualiko huu mkubwa na wa kihistoria,” alisema Kamwe na kuongeza kuwa.
“Julai 10, mwaka huu wachezaji wataanza kuingia kambini wote wapya na wazamani watakutana Avic Town, halafu sasa ndio watajua Pre Season itakuwa Avic au sehemu nyingine.”
Katika hatua nyingine, Kamwe aliongezea kuwa: “Mpaka sasa hivi tumemaliza usajili kwa msimu huu, wachezaji wote ambao tulikuwa tunawahitaji tayari wameshasaini, tumefunga zoezi la usajili, kinachofuatia ni kuwatambulisha na zoezi hilo litaanza baada ya utambulisho wa jezi mpya.”