Vicheko kwa watumiaji wa mafuta ya Petroli na dizeli Julai vitatawala kufuatia kushuka kwa bidhaa hizo katika mikoa inayochukua mafuta hayo bandari ya Dar es Salaam na Tanga ikilinganishwa na Juni.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inaonyesha kuwa bei za mafuta kuanzia Julai 5, 2023 yale yanayochukuliwa bandari ya Dar es Salaam petroli imeshuka kwa Sh137 kwa lita na kuwa Sh2,736 huku dizeli ikishuka kwa Sh118 kwa lita na kuwa Sh2,544.
Kwa mikoa ya kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) bei hiyo ya rejareja kwa mafuta ya petroli imeshuka kwa Sh188 kwa lita na kuwa Sh2,724 huku dizeli ikishuka kwa Sh58 kwa lita na kuwa Sh2,760.
Huku bei ikiendelea kusalia kwa mikoa ya kusini na ile inayochukua mafuta yake katika bandari ya Mtwara.
“Hakuna shehena ya bidhaa za mafuta iliyopokelewa kupitia Bandari ya Mtwara kwa Juni 2023. Hivyo basi, bei ya rejareja ya dizeli kwa mwezi Julai 2023 itaendelea kuwa ni ile iliyotangazwa katika toleo la tarehe 7 Juni 2023,”imesema taarifa hiyo.
Hata hivyo, Ewura imetoa angalizo la bei katika mikoa ya kusini endapo wafanyabiashara watalazimika kuchukua mafuta bandari ya Dar es Salaam, bei ya kikomo ya mkoa huo izingatiwe.
Aidha, Ewura imewaonya wafanyabiashara wa mafuta kuzingatia ukomo wa bei hivyo na kinyume na hapo hatua za kisheria zitachukuliwa.
“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo (Price cap) au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa (Floor Price) kama ilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ewura za Kupanga bei za mafuta za mwaka 2022,”imesema taarifa hiyo.