Elizabeth Sagati (23), mkazi wa Kijiji cha Sokoine wilayani Mvomero mkoani Morogoro, amemwaga machozi mbele vya viongozi wa dini wakati akisimulia jinsi alivyonusurika mara tatu kuozeshwa.
Elizabeth alitoa simulizi hiyo jana wakati wa uzinduzi wa mradi wa kupambana ukatili na ndoa za utotoni wa ‘Hapana marefu yasiyo na mwisho’.
Uzinduzi huo uliwashirikisha pia viongozi wa Serikali, Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa na ya nchini.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo unaotekelezwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Elizabeth alisema alihitimu darasa la saba mwaka 2013 akiwa na miaka 14, baba yake alipokea mahari na kutaka kumwozesha kwa mfugaji wa kijiji cha Sokoine, alipomweleza mama yake kuwa hataki alimsihi akubali.
“Kwa kuwa wanawake wa kimasai hawana sauti katika familia, mama alinishi nikubali, niliamua kukimbilia kwa mchungaji wa KKKT Usharika wa Sokoine na kumweleza changamoto hiyo.
“Aliambia (mchungaji) nirudi nyumbani, atanisaidia. Mungu alivyokuwa wa ajabu likatokea Kanisa la KKKT Morogoro likitafuta watoto wanaopitia mazingira magumu, nikachukuliwa na kwenda kusoma katika Shule ya Sekondari Image Lutheran, Iringa,” alisema Elizabeth.
Alisema alipomaliza mtihani wa kidato cha pili, alirudi nyumbani kusubiri matokeo, lakini alitekwa na vijana na kimasai (morani) walimchukua kwenye gari na kumpeleka kusipojulikana, lengo asiendelee na masomo. “Bahati nzuri nilikuwa nakumbuka namba ya simu ya mkononi ya matroni, nilimuomba simu dada aliyekuwa akinilinda, nikampigia na kumweleza kilichotokea.
“Viongozi wa dayosisi ya Morogoro walipopata taarifa walikwenda kwa baba na kumwambia kusudio la kumshtaki kama ataendelea kung’ang’ania niolewe,” alieleza.
Elizabeth alisema mama yake aliungana na viongozi wa kanisa akitaka aendelee kusoma, lakini baba yake aligoma. “Baada ya majadiliano ya muda mrefu, baba alikubali kwa shingo upande, lakini ugomvi uliendelea kati yake na mama na kusababisha watengane.” Alieleza kuwa hata matroni alipokwenda kumchukua na kumrudisha shule alikuwa amechelewa kwa kuwa wenzake walishaanza masomo ya kidato cha tatu muda mrefu, hivyo hakupokelewa.
Hali hiyo ilimfanya akae nyumbani kwa mwaka mmoja kabla ya uongozi wa kanisa kumtafutia Shule ya Kigurunyembe mkoani Morogoro alikosoma hadi kidato cha nne.
Elizabeth alisema baada ya kuhitimu, baba yake alitaka kumuozesha tena kwa mara ya tatu, lakini viongozi wa kanisa walimweleza watamfikisha kwenye vyombo vya sheria, hivyo alimuachia na kwenda kusoma katika Chuo cha Uandishi wa Habari Morogoro hadi alipotunukiwa diploma ya uandishi wa habari.
Alisema baadaye alijiunga na Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini, Dar es Salaam ambako anachukua Shahada ya Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia akiwa mwaka wa kwanza. “Nashukuru kanisa bila wao nisingekuwa hapa. Natamani shahada yangu ya pili nikasome nje ya nchi,” alisema Elizabeth huku akibubujikwa machozi.