Jeshi la Polisi limetoa maagizo kwa makamanda wa mikoa yote nchini kuhakikisha wanafanya doria katika barabara zote zitakazotumiwa na mabasi yatakayokuwa yanafanya safari zake saa 24 katika kudhibiti aina zozote za kihalifu.
Huo ni utekelezaji wa agizo lilotolewa, Juni 28, mwaka huu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akitoa hoja ya kuahirisha Bunge la Bajeti jijini Dodoma.
Alisema mabasi sasa yameruhusiwa kuanza safari zake usiku kwa sharti la wamiliki kuomba vibali.
Itakumbukwa mwaka 1992, aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela alisisitisha rasmi safari hizo kwa mabasi yote nchini.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano na vyombo vya habari, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji alisema makamanda hao watapaswa kushughulika zaidi na madereva wote watakao kuwa vinara wa uvunjaji wa sheria.
“Makosa hayo ni mwendokasi na kuyapita magari yaliyo mbele yao katika maeneo yasiyoruhusiwake. Watakabainika wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali ikiwemo kufungiwa leseni, tunataka madereva wenye nidhamu barabarani,”alisema.
Alisema kwa kuwa mabasi hayo yatakuwa yanasafiri usiku, madereva wanapaswa kuwa makini hasa kwa baadhi ya maeneo yenye barabara finyu, maeneo ya misitu minene, kona na giza kali.
Kamanda huyo alisema maeneo hatarishi yote yaliyobainishwa ikiwemo mlima Kitonga na yale yenye misitu mikubwa, polisi watakuwa wanafanya doria na operesheni za mwendelezo.
“Maeneo ambayo mara nyingi madereva huvunja sheria za usalama barabarani kama yenye miteremko inayosababisha ajali hasa usiku, yatakuwa kwenye uangalizi mkali na askari watakuwepo muda wote,”alisema Awadhi.
Ujumbe kwa abiria na wasafirishaji
Alisema ni wajibu wa watakaosafiri na mabasi hayo, kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kutoa taarifa watakapobaini kuna uvunjifu wa sheria utakao fanywa na madereva.
“Abiria wana nafasi kubwa ya kuona mwenendo wa madereva, wakiona mwendo ni hatarishi kwao, wasisite kutoa taarifa haraka ili hatua zichukuliwe kwa dereva husika,”alisisitiza.
Kuhusu wamiliki wa mabasi na wasafirishaji wengine, Kamishna Awadhi alisema wanatakiwa kuhakikisha wanasimamia vyombo vyao vya usafiri pamoja na madereva watakaokuwa wanaendesha huku akieleza kuwa wanao huo wajibu wa kuona sheria za usalama barabarani zikizingatiwa.
“Mmiliki au msafirishaji asije akabweteka akifikiri ni jukumu la Jeshi la Polisi peke yake, kwani anao wajibu wa kuona chombo chake kinachotoa huduma ya usafiri na dereva aliyepewa chombo, anasimamia sheria,”alisema.
Alisema wamiliki wanalojukumu la kuhakikisha wanawasimamia madereva wao wanakuwa na utimamu wa afya zao na kuwa na leseni zilizotolewa na mamlaka husika.
Wito kwa madereva
Alisema madereva watakaokuwa safarini hasa kwa wale wa masafa marefu, watapaswa kuwa na siha njema na utimamu wa mwili.
“Tunataka wawe na wajibu wa kufuata sheria za usalama barabarani kama walivyofundishwa darasani kwa maana anapokuwa barabarani takiwa na usukani, aongozwe na sheria,”alisema.
Latra kutoa ratiba
Awali, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Habibu Suluo alisema wataanza kutoa ratiba ya safari za mabasi hayo , baada ya kufanyika kwa kikao baina ya Wizara ya Mambo ya Ndani na ile ya Uchukuzi.
Wizara hizo zimeagizwa kukaa na kuweka mkakati unaokwenda kutekelezwa pindi safari hizo zitakapoanza hivi karibuni.
“Hatuna kipingamizi, tunachosubiri ni hicho kikao kifanyike, tutaanza kutoa ratiba inayoonyesha utaratibu mzima utakavyokuwa,” alisema Suluo.
Mabasi ya Newforce kusitishiwa ratiba za usiku
Katika hatua nyingine, Saluo alisema Latra imesitisha ratiba za mabasi 38 ya Kampuni ya New force yaliyokuwa yanafanya safari zake kuanzia saa 9:00 na saa 11 alfajiri na kurejeshwa saa 12:00 asubuhi.
Alisema kuanzia kesho, mabasi hayo yataanza safari zake saa 12:00 asubuhi na kuendelea.
Alisema hiyo ni baada ya mabasi matano ya kumpuni hiyo kupata ajali mfululizo ndani ya wiki nne.
Hata hivyo, alisema hiyo si adhabu, bali ni utaratibu wa kutaka kudhibiti hali hiyo na kuhakikisha usalama wa abiria.
“Kutokana na wimbi la ajali kwa mabasi haya, tulifanya uchunguzi na kubaini uvunjaji wa sheria kwa makusudi unaofanywa na madereva wake ndiyo umechangia kutokea kwa ajali hizi, hivyo tumesitisha ratiba zao za usiku na kuzirudisha zianzie Saa 12:00 asubuhi,” alisema.
Akizungumzia hilo, Meneja wa Kampuni ya New Force, Masumbuko Masuke alisema kabla ya mamlaka kusitisha ratiba yao, nao pia walipanga kupunguza magari ili wafanye tathimini.
“Hizi ajali zilizotokea zimetupa hasara kubwa, tulipanga kuanzia Jumamosi ijayo tupunguze mabasi tubakiwe na machache tutakayo mudu kuyasimamia,” alisema Masuke.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri (Latracc) Ngowi Leo alisema hatua iliyochukuliwa na Latra inatia matumaini kwa usalama wa abiria.