Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Jomari Satura, ameamua kumvua madaraka Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Kivule kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano, Tabu Shaibu, hatua hiyo imefikiwa baada ya Mganga huyo kushindwa kusimamia na kuhakikisha utoaji wa huduma za afya katika kituo hicho unazingatia ubora, miongozo, taratibu na sheria za afya.
Kupitia taarifa yake Mkuu wa Kitengo cha Habari Tabu Shaibu ameeleza kwamba Ofisi ya Mkurugenzi inakemea vikali vitendo kama hivi na itahakikisha havijirudi tena na kuwataka watumishi wote wa sekta ya afya na sekta nyingine kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia miongozo na taratibu zote,
Hatua hiyo inakuja baada ya kusambaa kwa video iliyomuonyesha mtumishi wa hospitali hiyo akisafisha na kuanika juani vifaatiba nje ya jengo la hospitali, kitendo ambacho hakikubaliki kwa kuwa ni kinyume na taratibu na miongozo ya afya.
Aidha, Kwa niaba ya uongozi wa jiji, Satura ameomba radhi kwa mamlaka na umma wote wa Watanzania kwa kitendo hicho kilicholeta usumbufu na taharuki.