Mkutano wa wajumbe zaidi ya 200 wa Kanisa Katoliki Tanzania umeibua mitazamo tofauti kuhusu uwezekano wa watu wenye ulemavu kuingia katika malezi ya wito wa utawa na upadri.
Mjadala huo uliibuka wiki hii wakati wa kongamano la maadhimisho ya miaka 60 ya Konstitusio ya Liturujia Takatifu, baadhi wakieleza changamoto zinazoweza kukwamisha kundi hilo wakati wa utumishi wao.
Katibu wa Jimbo la Zanzibar, Beatrice Milinga ndiye aliyeibua hoja hiyo akishauri kanisa kuondoa kikwazo kwa watu wenye ulemavu wanaotaka kutumia wito wao katika nafasi za utawa na upadri.
Beatrice alikuwa miongoni mwa wajumbe hao kutoka majimbo 34 waliotathmini utekelezaji wa Hati ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano wa mwaka 1963, inayoweka msingi wa kuboresha maadhimisho ya ibada mbalimbali.
Hoja hiyo inaibuliwa wakati Sheria za Kanisa (Canon Law) za mwaka 1983, zikielekeza utaratibu wa kupokea, kulea na kutoa daraja la upadri na utawa kwa watu watakaokuwa na sifa kutokuwa na tatizo la kiafya, utasa na awe amekamilika kimwili na kiroho katika utashi wake.
“Kanisa linatufundisha umuhimu wa kuinua wito wa watoto katika jamii. Sasa kuna watoto wengi wenye ulemavu tunawafundisha na wanatamani pia kuingia kwenye wito wa upadri na utawa, lakini wanakwama kwa sababu ya hali zao, nadhani tunaweza kulitazama hilo,” alisema Beatrice.
Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na baadhi ya washiriki, huku Dk Camillus Kassala ambaye ni mkurugenzi wa hadhi ya utu wa binadamu, idara ya haki, amani na uadilifu wa baraza hilo akifafanua mazingira matatu yanayotengeneza mazingira magumu ya ushiriki wao.
“Kuhusu nafasi ya watu wenye ulemavu kuwa katika wito wa maisha ya kitawa au upadri, kimsingi lazima kuwe na masharti matatu,” alisema Dk Kassala.
Alisema uwezekano wa kutumikia fursa hiyo utategemea kanuni, utaratibu, vigezo vya shirika au jimbo husika litakalomtazama utayari wake.
Dk Kassala alisema sharti la pili linalofanikisha au kukwamisha wito wake ni sadaka aliyonayo, inayomtaka kuwa na utayari wa kukubali au kukataa baadhi ya haki za msingi anazostahili mtu mwingine katika maisha.
“Bila sadaka huwezi kuwa padri au mtawa, sharti la tatu linategemeana na shughuli atakazopewa na shirika au jimbo, kwa kuwa shughuli nyingi zinafanikishwa na watu wenye viungo kamili, kigezo hiki cha tatu kinaweza kuwa kigumu kupokewa na wenye ulemavu. Kwa hiyo, kwa ufupi naweza kusema hayo kuhusu nafasi ya watu wenye ulemavu,” alisema Dk Kassala.
Padri Gerald Gabriel alifafanua mazingira magumu ya kuwapokea watu wenye ulemavu, akifananisha na ilivyo vigumu kwao kufanya kazi jeshini.
Naye Padri Titus Amigu, mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), alisema kitendo cha kuwapokea katika wito huo kinaweza kubadili nia njema inayokusudiwa.
Alisema mazingira ya kazi za wito huo ndiyo yanatengeneza kikwazo cha kupokewa kwao.
“Badala ya kumsaidia ili atumikie wito wake unaweza kukutana na changamoto nyingine mpya ya kukiuka haki zake,” alisema Padri Amigu.
Mtawa Joyce Mboya kutoka Idara ya Elimu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alisema wito huo unahitaji watu wasiokuwa na tatizo la kimaumbile kutokana na changamoto wakati wa utumishi wake.
“Inahitaji uwe tayari kufanya kazi mahali popote na mazingira yoyote, hatua ambayo ni ngumu kwao,” alisema.