Jeshi la Polisi Nchini limesema kuwa limeendelea kutekeleza Mapendekezo ya tume ya Haki Jinai katika nyanja mbalimbali hapa nchini.
Akitoa taarifa hiyo Leo Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime amesema Miongoni mwa Mapendekezo hayo ni pamoja na kubuni miradi katika utekelezaji wa Polisi Jamii ili kuendelea kutoa elimu na kuwa karibu zaidi na jamii.
DCP Misime ameongeza kuwa Jeshi la Polisi nchini lingependa kutoa taarifa kuwa mbali na miradi takribani 23 inayotekelezwa, pia, limebuni kampeni ya kuendelea kuishirikisha jamii katika kuzuia ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto itakayobebwa na kauli inayosema ‘TUWAAMBIE KABLA HAWAJAHARIBIWA’.
Aidha amebainisha kuwa Kampeni hii italenga zaidi watoto wa kidato cha kwanza, kidato cha tano pamoja na wanachuo wa mwaka wa kwanza ambapo imejikita zaidi katika kuwapatia elimu ili kuwajengea uelewa walengwa hao na kujitambua zaidi.
Sambamba na hilo ameweka wazi kuwa Kampeni hiyo itakuwa ni ya nchi nzima ikiendeshwa na Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto na inatarajiwa kuzinduliwa rasmi huko mkoani Njombe, Agosti 29, 2024 ambapo Kamishna wa Polisi Jamii kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma, CP Faustine Shilogile atashiriki katika uzinduzi huo pamoja na wageni mbalimbali.
Misime amesema kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka.