WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wahandisi wazawa kuhakikisha miradi wanayoisimamia inakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa na iendane na thamani ya fedha inayotumika.
Amesema ni wajibu wa Wahandisi kuisaidia Serikali kuokoa fedha kwa kukadiria fedha inayohitajika kulingana na thamani ya mradi husika.
Ameyasema hayo 27, Agosti 2024 alipomuwakilisha Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za Kuadhimisha Miaka 50 ya Idara ya Ujenzi ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) zilizofanyika katika ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip, Zanzibar
“Uhandisi ni taaluma yenye miiko na inayopaswa kuzingatia maadili. Miongoni mwa miiko na maadili hayo ni kuhakikisha kuwa miradi mnayoisimamia inakidhi viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa na inaendana na thamani ya fedha inayotumika.”
Aidha, amewataka waajiri wote nchini kuweka utaratibu wa kuajiri wahandisi wahitimu wa ndani na kuwajengea uwezo wakati wakiwa kazini pamoja na kushirikiana na taasisi za mafunzo kutenga nafasi na kuwapokea vijana waliopo mafunzoni ili kuwapatia uzoefu wa kazi.
“Utaratibu huu ni kwa manufaa ya Taifa na kwa waajiri pia kwa kuwa vijana watahitimu wakiwa wameiva kitaaluma na kiutendaji.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Taasisi ya Sayansi ya Teknolojia ya Karume na taasisi nyingine za mafunzo nchini zihakikishe zinazalisha wahitimu wengi wenye maarifa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira ili kuongeza kiwango cha kazi za kibobezi zinazofanywa na wazawa.
Kwa Upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Lela Mohamed Mussa (MB), amesema wameanzisha programu ya kutoa fedha kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa fani za Uhandisi na kutoa ufadhili na mafunzo ya amali pamoja na kutoa kipaumbele kwa wanafunzi wa fani hiyo.
Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Adolf Mkenda amesema Wizara zote zimekuwa na Ushirikiano wa kuwezesha wanafunzi wa fani za Uhandisi ili kuongeza tija katika mafunzo wanayopata.