Israel imekubali kusitisha mapigano huko Gaza ili kuruhusu utoaji wa chanjo ya watoto dhidi ya polio, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema.
Kampeni hiyo italenga kutoa chanjo kwa watoto 640,000 kote katika ukanda wa Gaza na itaanza Jumapili, afisa mkuu wa WHO Rik Peeperkorn alisema.
Itatolewa katika hatua tatu tofauti, sehemu za kati, kusini na kaskazini za ukanda huo.
Katika kila hatua, mapigano yatasitishwa kwa siku tatu mfululizo kati ya 06:00 na 15:00 saa za eneo hilo.
Makubaliano hayo yanafikiwa siku chache tu baada ya maafisa wa Umoja wa Mataifa kusema mtoto wa miezi 10 alikuwa amepooza kwa kiasi fulani baada ya kisa cha kwanza cha maambukizi ya polio huko Gaza katika kipindi cha miaka 25.
Takriban dozi milioni 1.26 za chanjo ya polio yenye kutolewa kwenye mdomo aina ya 2 (nOPV2) tayari iko Gaza, na dozi 400,000 za ziada zinatarajiwa kuwasili hivi karibuni.