Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Mara, Simiyu na baadhi ya halmashauri za mkoa wa Manyara utafanyika kwa siku saba kuanzia kesho tarehe 04 hadi 10 Septemba, 2024 ambapo jumla ya wapiga kura wapya 491,050 wanatarajiwa kuandikishwa.
Kwa mujibu wa makadirio yaliyofanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na ambayo yanatokana na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya wapiga kura 3,391,017 wanatarajiwa kuwemo kwenye Daftari la Kudumumu la Wapiga Kura kwenye mikoa hiyo wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhan idadi hiyo inaweza kuongezeka zaidi.
“Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha kuwa wapiga kura,” amesema Bw. Kailima.
Kwenye uboreshaji huo wa Daftari jumla ya vituo 4,373 vitatumika kuwaandikisha wapiga kura wapya na kuboresha taarifa za wapiga kura walioandikishwa kwa miaka iliyopita.
Uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo unafanyika ikiwa ni mwendelezo wa zoezi hilo lililozinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa mkoani Kigoma tarehe 20 Julai, 2024 ambapo mzunguko wa kwanza ulijumuisha mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora.
Baada ya uboreshaji kukamilika kwenye mikoa hiyo ulifuata mzunguko wa pili kwenye mikoa ya Kagera na Geita na wa tatu kwenye mikoa ya Mwanza na Shinyanga.
Mzunguko wa nne wa uboreshaji wa Daftari unajumuisha mkoa wa Mara, baadhi ya halmashauri za Mkoa wa Manyara ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Babati na Halmashauri za Wilaya za Babati, Hanang na Mbulu na mkoa wa Simiyu ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.