Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo Jumatano Septemba 11, 2024 anatarajiwa kuzindua tathimini huru na ya kina ya miaka mitano ya utekelezaji wa mpango wa kuboresha Mazingira ya Biashara nchini Tanzania.
Septemba 11, 2024, akiwa Jijini Arusha kwenye Kituo cha Uwekezaji (TIC) Kanda ya Kaskazini, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amewaambia wanahabari kuwa zoezi la uzinduzi huo litafanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar Es salaam kuanzia majira ya saa kumi na moja jioni.
Prof. Kitila amesema mpango huu ulikuwa na lengo la kufanya uchambuzi wa mazingira ya biashara nchini na kuanisha mageuzi na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kutatua changamoto na kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini Tanzania.
Mhe. Waziri Mkuu pia amepangiwa kuzindua Taarifa ya Hali ya uwekezaji nchini kwa mwaka 2023, Mwongozo wa uanzishaji na uendeshaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi (Special Economic Zones)pamoja na kuzindua mpango Mkakati wa Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji.