MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imetishia kusitisha safari za usiku kwa mabasi yanayokiuka masharti, kanuni na taratibu za usafirishaji.
Ukiukwaji wa kanuni hizo umeelezwa kuwa ni chanzo cha ajali, vifo na majeruhi kwa abiria.
Kadhalika, mamlaka hiyo imetoa siku saba kwa mabasi ya Super Feo, Abood na BM kujirekibisha kabla hayajasitishiwa leseni za kutoa huduma baada ya kubainika kukiuka masharti kutokana na kusababisha ajali mfululizo.
LATRA pia imesitisha utoaji huduma kwa mabasi yote ya Katarama kwa muda usiojulikana mpaka kazi ya kuyachunguza itakapokamilika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo, mabasi ya Katarama yanatuhumiwa kufanya hujuma ya kuchezea mifumo ya kufuatilia mienendo ya mabasi (VTS) na mifumo ya kutoa taarifa (I. Button) na kufunga vifaa vyake ambavyo havijulikani ni vya modeli gani na si vile ambavyo vimethibitishwa na Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS).
Suluo alitoa uamuzi huo jana kwa waandishi wa habari baada ya kikao chake na baadhi ya wamiliki wa mabasi ya masafa marefu yenye uwekezaji mkubwa katika eneo hilo ambayo hivi karibuni yameonekana kufanya makosa na kupata ajali mfululizo kwa mabasi ya BM, Super Feo na Abood.
“Mtakumbuka kwamba tunakaribia kutimiza mwaka mmoja tangu tuanze safari za usiku. Serikali ilifanya uamuzi kupitia Mkutano wa 11 wa Bunge, Juni 28, mwaka jana kutoa ruhusa kwa mabasi kusafiri nyakati za usiku na ilitoa maelekezo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi kuweka utaratibu wa kutumia kwenye safari hizo za usiku.
“Tangu kipindi hicho mpaka Septemba mwishoni taratibu ziliaanza kuwekwa na sisi kama Wizara ya Uchukuzi tulianza kushirikiana na wadau wetu na hasa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), ili kuweka utaratibu na mojawapo tulizoweka ni kuwataka watoa huduma wasaini tamko la kukubali masharti ya leseni wanaposafiri usiku,” alisema Suluo.
Alisema yako masharti saba ambayo wasafirishaji hao walikubali na kuyatia saini kwa ajili ya kupewa kibali cha kutoa huduma ya usafirishaji usiku na kwamba, ili kukidhi kupewa kibali hicho walitakiwa wayakubali na wayasaini lakini baadhi yao licha ya kufanya hivyo tayari wameanza kuyakiuka.
Alitaja masharti hayo kuwa ni pamoja na kutia saini tamko hilo la LATRA na kulikubali, kuunganisha mabasi kwenye VTS, madereva kupokezana kwenye safari za zaidi saa nane, madereva kusajiliwa na kuthibitishwa na kupewa kifaa utambuzi (I,botton).
Mengine ni kuwa na ofisa mahsusi ambaye jukumu lake ni kufuatilia mabasi ya kampuni yake, kutoa taarifa sahihi za abiria wanaosafiri, mizigo kuwekwa alama ya utambulisho ya mhusika, kutoruhusu asiye abiria kupanda kwenye gari kabla na wakati wa safari.
“Kwa hiyo baadhi wameanza kukiuka masharti hayo na sisi kama LATRA kwa mamlaka tuliyopewa na sheria, tunatakiwa kuwalinda Watanzania, hatuwezi kuvumilia kuona masharti haya yanakiukwa.
“Hizi ajali zinavyotokea ndugu zangu, vifo, majeruhi havikubaliki, mtu mmoja tu akifa kwenye ajali hata muuze mabasi yote ya nchi hii kurudisha roho ya yule aliyefariki kutokana na ajali haiwezekani, kwa hiyo tusifurahie au kuona ajali imetokea halafu eti mnasema amefariki mtu mmoja tu, hiyo roho ya mtu mmoja ina thamani kuliko mabasi hayo yote, mtu asikie uchungu ndani yake kwamba ninapoteza uhai wa mtu kwa biashara yangu,” alisema.
Kuhusu mabasi ya Katarama, Suluo alisema tayari LATRA imelikabidhi Jeshi la Polisi kazi ya kufanya uchunguzi na uamuzi kuhusu uendeshaji wa huduma kwa mabasi yake utatolewa baada ya kumalizika kwa uchunguzi.
“Mwaka jana pia tulimsimamisha kutoa huduma mwezi mzima, mwaka huu tena tumemsimamisha kwa sababu ana vurugu barabarani, amechezea kifaa cha kufuatilia mienendo ya mabasi yake, ameweka kifaa chake ambacho hakieleweki ni ‘Modeli’ ya wapi maana siyo kile ambacho kimethibtishwa na mamlaka za nchi yetu yaani TBS na hakitumi taarifa kwetu, kwa hiyo kwenye mwendo anakwenda hadi zaidi ya 180, ila kwenye mfumo hatupati.
“Na amebadili na kuharibu antena kwa hiyo inakuwa haitupi ile taarifa tunayoitegemea, huyu mtu hatuwezi kumvumilia, tumeamua kusitisha leseni ya usafirishaji kwenye mabasi yake yote kuanzia sasa mpaka tumfanyie uchunguzi, na kazi hii itafanywa na Jeshi la Polisi.
“Kwa hiyo tunaomba abiria wasitumie mabasi yake popote pale kwa sababu ni hatari kwao mpaka uchunguzi utakapokamilika na kuamua vinginevyo, hatutakubali kuhatarisha maisha ya Watanzania,” alisema Suluo.
Mwenyekiti wa TABOA, Abdallah Kiongozi, alisema chama hicho hakiko tayari kumtetea msafirishaji anayekwenda kinyume cha taratibu za LATRA, na kutaka wajirekebishe kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa.