KUNDI la lenye uhusiano na Al-Qaeda Jumanne lilidai kuhusika na shambulizi baya katika mji mkuu wa Mali, Bamako, ambapo wapiganaji wa kundi hilo walidhibiti kwa muda sehemu ya uwanja wa ndege wa kimataifa.
Picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya mawasiliano ya kundi la Jama’at Nusrat al-Islam wal Muslimeen (JNIM) zilionyesha wapiganaji wakizunguka-zunguka na kufyatua risasi hovyo kwenye madirisha ya jumba anakopita rais katika uwanja wa ndege.
Ofisi ya mkuu wa jeshi la Mali baadaye ilisema kwamba shambulizi hilo liliua wanajeshi kadhaa lakini haikutoa maelezo zaidi kuhusi idadi ya waliokufa.
Ilithibitisha kwamba kituo cha mafunzo kwa askari polisi na uwanja wa ndege wa mji mkuu vililengwa.
Jumba hilo lililoshambuliwa kawaida linapokea wageni rasmi na rais wa taifa hilo la Afrika Magharibi, ambalo liko chini ya utawala wa kijeshi tangu mapinduzi ya 2020 na 2021.
Video moja ilionyesha mpiganaji akifyatua risasi bila wasiwasi kwenye injini ya ndege, huku katika video nyingine moshi mwingi ukionekana kutoka uwanja wa ndege na kwenye jumba kunakotua ndege ya rais.
“Shambulizi hili la kikatili na la kiuhaini lilisabisha vifo upande wa wanajeshi wetu, wakiwemo baadhi ya askari polisi waliokuwa katika mafunzo,” ofisi ya mkuu wa jeshi ilisema katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa, na kuongeza kuwa shambulizi hilo lilizimwa.
Taarifa hiyo ilisema “hali ilidhibitiwa kwa haraka.”
JNIM ilisema kwenye mitandao yake ya mawasiliano kwamba “operesheni maalum” ililenga uwanja wa ndege wa kijeshi na kituo cha mafunzo kwa askari polisi katika mji mkuu wa Mali nyakati za alfajiri.