Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameielekeza Halmashauri ya Jiji la Arusha kuweka mpango wa uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Mhe. Mchengerwa ameyasema mara baada ya kukagua ujenzi wa majengo ya wagonjwa wa nje (OPD Complex) katika Kituo cha Afya Levolosi na Hospitali ya Jiji la Arusha iliyopo eneo la Njiro.
Amesema uboreshaji wa miundombinu ya afya unatakiwa kuwa na viwango vya kimataifa ili kuendana na mahitaji ya ndani na nje ya nchi.
“Tunahitaji kuona uwekezaji katika huduma za afya unakuwa na viwango vya kimataifa ili wananchi wetu wa ndani na wageni kutoka mataifa mbalimbali ambao kwa sasa wanatembelea nchini wamekuwa wakitembelea nchini na wakipata changamoto za afya za afya wanakimbizwa kwa hospitali za nje lakini tukiwa na huduma bora hapa jijini tutaweza kuwahudumia mpaka watalii.”
Ujenzi wa jengo la kisasa la wagonjwa wa nje katika Kituo cha Afya Levolosi unagharu zaidi ya Sh bilioni 3.5.
“Fedha zilizotolewa hapa ni nyingi, kiasi kama hiki kwa maeneo mengine zinajenga Hospitali ya Wilaya kwa hiyo jengo hili linatakiwa kuwa bora na lenye uwezo wa kutoa huduma zote muhimu ambazo wageni na wenyeji wanaweza kuzihitaji.”
Kuhusu jengo la OPD Complex linalojengwa Hospitali ya Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa gharama ya Sh bilioni 17, Mhe. Mchengerwa alitaka fedha hizo kuleta mapinduzi katika upatikanaji wa huduma za afya katika Jiji la Arusha.
“Lengo la kuongeza miundombinu ya hospitali hizi ni ili kuboresha utoaji wa huduma za afya katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kutoa huduma za kibigwa na ubingwa kibobezi hivyo kuwa sehemu ambayo wageni wanaweza kufanya utalii wa kimatibabu.”
Mhe. Mchengerwa pia amewatala uongozi wa halmashauri hilo kuingia mikataba na kampuni za kitalii zinazoleta watalii kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa wageni wanaotembelea jiji hilo endapo watapata changamoto za kiafya.