Msimamizi wa Uchaguzi wa serikali za Mitaa kwa mwaka 2024 kwenye Halmashauri ya Jiji la Dar Es salaam Bw. Elihuruma Mabelya amehimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuanzia leo Ijumaa Oktoba 11, 2024 ili kujiandikisha kwenye daftari la Mkazi na kupata sifa za kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 ya mwaka huu.
Msimamizi huyo wa Uchaguzi ambaye amekuwa akiwatembelea wananchi wa maeneo mbalimbali ikiwemo MnaziMmoja na Banana Jijini Dar Es salaam kutoa elimu kuhusu uchaguzi huo, amesema ni muhimu wananchi kuitambua haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa mustakabali wa maendeleo ya mitaa yao kwa miaka mitano ijayo.
Mabelya kwa upande mwingine amewahakikishia wananchi kuwa wamejipanga kikamilifu katika zoezi la uandikishaji wapigakura kwenye daftari la mkazi linaloanza leo Oktoba 11 mpaka Oktoba 20, 2024 akisema lengo ni kuhakikisha kuwa mwananchi anatumia muda mfupi zaidi katika kujiandikisha ili kutokumkwamisha kuendelea na shughuli zake za uzalishaji mali.
Chanzo – Global Pulishers