“Kitakacho tutofautisha sisi na wao si uwezo wa kufikiri bali uwezo wa kuamua lililo sahihi baada ya kufikiri. Maana hata mpumbavu hufikiri, ila shida ni je anafikiria lililo sahihi?” JULIUS KAMBARAGE NYERERE (1922-1999).
Ni leo nyingine ikiwa ni miaka 25 ambayo imewasili bila ya uwepo wa Baba wa Taifa na muasisi wa Taifa la Tanzania, Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye alifanya mengi yaliyoacha alama kwa Taifa hili na yasiyofutika, kutokana na umahiri wake wa uongozi na busara alizojaaliwa na mwenye enzi MUNGU wakati wa uhai wake.
Kuna mengi ya kujifunza juu yake lakini hapa nakuletea taswira halisi ya mtanzania huyu msomi kwenye mchango wa Taifa hili kielimu, kisera, kiuchumi na kiuongozi, kwa kuzingatia kauli ya Hayati baba wa Taifa Julius K. Nyerere kwamba “Taifa lisilo na utamaduni wake ni Taifa mfu.”
Nakumbuka niliwahi kusimuliwa na Mwalimu wangu Doto Bulendu kuwa, miaka ya 1960-1970 Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kulikuwa na jarida maarufu lililoitwa CHECHE ambalo lilikuwa na kauli mbiu ya “Jifunze Kupambana, Pambana Kujifunza” likisheheni maandiko yaliyozua mijadala mikali yenye hoja zenye mashiko.
Aghalabu, Jarida hili lilikosa hoja zisizo kinzani juu ya falsafa na sera za nchi, kwani wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, kwa sehemu kubwa walikuwa wanaandika makala zenye kuchambua sera na kuziangalia kama kweli zinaweza, kufanikisha ujenzi wa nchi ya ujamaa na kujitegemea.
Katika ukumbi ule wa Nkrumah, wenyewe ulikuwa hauishi mijadala mikali juu ya mwelekeo wa nchi na mara nyingi Mwalimu Nyerere alikuwa akifika hapo kusikiliza mijadala na hata kutoa mihadhara na kujibu hoja juu ya falsafa na sera za nchi ambazo serikali yake ilikuwa inaziamini.
Hata hivyo, wakati fulani Mwalimu alialikwa Nkrumah kujibu hoja za wasomi hao, huku akielewa fika kuwa hoja zao zilikuwa zinapigia chapuo falsafa za Karl Max na katika kuwashangaza aliwaambia “kama Karl Max angezaliwa Sumbawanga, basi angeandika kuhusu azimio la Arusha.” iliwastaajabisha.
Mwalimu Nyerere, kwa miaka hiyo alijenga utamaduni wa kuhakikisha kila Kiongozi Mkuu wa nchi anayefanya ziara nchini anapewa fursa ya kwenda kutoa mhadhara chuo kikuu cha Dar es Salaam akiamini kuwa Chuo Kikuu ndiyo sehemu pekee ambapo mustakabali wa nchi unajengwa.
Baba huyu wa Taifa pia aliamini kuwa, Chuo Kikuu ndiyo sehemu pekee ambayo mawazo mapya huzaliwa na pia ni sehemu ambayoipo mijadala mbalimbali yenye kustawisha mustakabali wa maendeleo ya nchi.
Lakini kwasasa hali ni tofauti, kutokana na mabadiliko makubwa ya Viongozi wa sasa na si kwa Tanzania pekee, bali hata nchi nyingine za barani Afrika, Viongozi wengi wa Serikali wapo mbali na vyuo vikuu, hawafiki hapo kutetea sera zao na vyuo vikuu vingi barani Afrika kwasasa vinaonekana ‘sio dili’.
Tukiuangalia msingi wa ujenzi wa chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ulikuwa ni kuzalisha jamii ya vijana wadadisi, wanaohoji mambo kwa tafiti na takwimu, wanaotoa mwelekeo wa nchi bila woga na wasio ndumilakuwili.
Na bila shaka hili halina ubishi kuwa ni lazima vyuo vikuu vibaki kuwa msingi wa maendeleo ya nchi, Viongozi wetu wajenge tabia ya kwenda vyuo vikuu ili kuongea na vijana kwa kushirikiana kuchambua sera zitakazosaidia kuleta matokeo chanya katika nyanja mbalimbali za ukuzaji wa nchi.
Vyuo vikuu vingi vya Tanzania, vinaonesha dalili ya kugubikwa na matamasha ya wanamuziki, leo ukitembelea huko utakutana na matangazo ya matamasha ya wasanii au sherehe za aina nyingi zisizo na afya kwa maendeleo ya nchi na si mijadala kuhusu mustakabali wa Taifa.
Muda umefika wa kuyakumbuka mema yote aliyoyafanya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kuanzisha utaratibu wa kwenda vyuo vikuu na kuzungumza na wasomi, kuwaeleza ni aina gani ya Tanzania tunayotaka kuijenga, wasomi watuambie kuhusu sera za nchi yetu na kama zinaweza timiza azma ya kuijenga Tanzania, kama utamaduni tuliouzoea hapo awali.
Tukumbuke kwamba, Mwalimu Nyerere aliipenda Tanzania kwa dhati, aliliweka Taifa hili katika ramani ya dunia, akaliheshimisha kama taifa huru, akajenga umoja na mshikamano, akaimarisha mifumo bora ya utawala, akatulea kama watoto wa Baba mmoja, hivyo ni vyema tukauenzi utamaduni wetu uliopotea.
NYERERE NI NANI?
Julius Kambarage Nyerere, alizaliwa mwaka 1922 katika kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara, nchini Tanzania (wakati ule ikiitwa Tanganyika), akiwa mmoja kati ya watoto 26 wa Nyerere Burito, (Chifu wa kabila la Wazanaki).
Wakati wa utoto wake (akiwa na miaka 12), Nyerere aliwahi kuchunga mifugo ya baba yake na wakati huo pia alianz masomo shuleni akitembea umbali wa kilomita 30 hadi Musoma mjini ambapo baada ya kumaliza shule ya msingi aliendelea kusomea shule ya wamisionari Wakatoliki mkoani Tabora, (sasa Tabora Boys).
Akiwa na umri wa miaka 20 Mapadri wakiona akili yake kubwa walimsaidia kusomea ualimu katika chuo cha Makerere kilichopo Kampala nchini Uganda kuanzia mwaka 1943 hadi 1945 na hapo alianzisha tawi la Umoja wa Wanafunzi Watanganyika, akijihusisha pia na tawi la Tanganyika African Association (TAA).
Baada ya kumaliza masomo ya ualimu, alirudi Mkoani Tabora akifundisha shule ya St. Mary (sasa Milambo High School) na mwaka mwaka 1949 alipata nafasi ya kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Edinburgh na kuwa (Mtanganyika wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza na wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanganyika).
Aliporejea kutoka masomoni, alifundisha Historia, Kiingereza na Kiswahili katika shule ya St. Francis (sasa Pugu Sekondari) ya jijini Dar es Salaam na mwaka 1953 alichaguliwa kuwa rais wa chama cha Tanganyika African Association (TAA), chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere.
Mwaka 1954, alibadilisha jina la chama cha TAA kuwa chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA na ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kikawa tayari chama cha siasa kinachoongoza nchini Tanganyika.
Uwezo wa Mwalimu Nyerere, uliwashtua viongozi wa kikoloni na kumtaka kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu hapo Nyerere akalazimika kujiuzulu ualimu na kuzunguka nchi nzima ya Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta umoja katika kupigania uhuru.
Badaye akapata pia nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya TANU katika Trusteeship Council na Fourth Committee ya Umoja wa Mataifa (UN), jijini New York nchini Marekani.
Uwezo wake wa kuongea na wa kuunganisha watu ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila umwagaji wa damu na ushirikiano mzuri aliouonesha kwa aliyekuwa gavana wa wakati huo, Richard Turnbull, ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania), mwaka 1961.
Heri kwako na siku njema ya Nyerere Day.