Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wanachama wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) kuvumbua njia zinazotekelezeka katika kuhamisha teknolojia zitakazowasaidia vijana ambao ni idadi kubwa ya Watanzania kwa sasa.
Makamu wa Rais amesema hayo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe ya Kufunga Mwaka ya CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) iliyofanyika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam. Amesema ni muhimu kuwasaidia vijana katika teknolojia za kijani, kuunga mkono katika tafiti na maendeleo pamoja na kuanzisha vituo atamizi vya teknolojia.
Amewasihi kupitia upya vigezo vya kujiunga na CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) ili kuongeza idadi ya vijana kutoka biashara zinazochipukia kama vile masuala ya burudani, tehama na michezo.
Aidha Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) kahamasisha wanachama wao kuipa kipaumbele ajenda ya mabadiliko ya tabianchi. Amewasihi kuongeza jitihada katika ushirikiano na suluhu za kibunifu ambazo zitahusianisha shughuli za Taasisi zao na malengo ya Taifa ya uhifadhi wa mazingira pamoja na kutumia fursa zinazotokana na uhifadhi.
Vilevile Makamu wa Rais Amesema unahitajika ushirikiano baina ya Serikali na Sekta Binafsi katika kutafuta mwelekeo sahihi kuelekea uchumi wa kijani ambao unaunga mkono maendeleo endelevu na kuendana na vipaumbele vya Taifa.
Pia, amesema wakati Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana ikiwemo kubadili mitaala itakayowezesha kuendana na soko la ajira, CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) inapaswa kuongeza wigo wa shughuli zake ili kuongeza ajira zaidi, kutoa mafunzo kwa vitendo na mitaji kwa biashara zinazochipukia kwa wahitimu.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo mabadiliko ya sera na miundo ya kitaasisi ili kudhibiti urasimu pamoja na rushwa na hivyo kuchagiza sekta binafsi shindani. Ameongeza kwamba serikali imeimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuhamasisha diplomasia ya uchumi ili kulifanya Taifa kuwa kiungo muhimu kikanda na kimataifa pamoja na kuvutia uwekezaji kutoka mataifa ya nje. Ametoa wito wa kuongeza ushirikiano wa kibunifu baina sekta binafsi na serikali katika kuchochea mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini.