Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limeanza mwaka 2025 kwa mafanikio, likitoa ripoti ya usimamizi bora wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya ambazo zilifanyika kwa amani na utulivu. Pamoja na hilo, sheria za usalama barabarani zilisimamiwa kikamilifu ili kupunguza ajali.
Katika kipindi cha sherehe hizo, jumla ya madereva 179 walikamatwa na kupimwa kiwango cha ulevi. Kati yao, madereva 30 walikutwa na kiwango cha ulevi zaidi ya miligramu 80, huku 22 wakitokea Wilaya ya Kinondoni, 6 Wilaya ya Ilala, na 2 Wilaya ya Temeke.
Jeshi hilo limechukua hatua kali kwa kuwafungia leseni za udereva kwa miezi 6 kwa mujibu wa kifungu 28 (3)(b) cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 iliyorekebishwa mwaka 2002.
Katika kipindi cha Novemba hadi Desemba 2024, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kufanikisha kesi kadhaa mahakamani. Baadhi ya matukio yaliyojulikana ni:
Sadick Foreni (30), mkazi wa Mbagala, alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kulawiti katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke.
Joseph Ferdinand (35), mkazi wa Mbagala Kibonde Maji, pia alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kulawiti, Ayub Hatibu (32), mkazi wa Tabata, alihukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la kubaka katika Mahakama ya Wilaya ya Kinyerezi.
Salmin Athuman (30), mkazi wa Kitunda, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 kwa unyang’anyi wa kutumia silaha, Henry Peter (36), mkazi wa Mbezi, alihukumiwa miaka 30 kwa kosa la kubaka katika Mahakama ya Wilaya ya Ubungo.
Ramadan Amir (30), mkazi wa Kawe, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Kuzuia uhalifu na dawa za kulevya Jeshi la Polisi limeendelea kufuatilia kwa karibu makundi yanayojihusisha na uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya. Katika juhudi hizi, watuhumiwa 250 walikamatwa kwa tuhuma za kuuza, kusafirisha, na kutumia dawa za kulevya.