Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia John Isaya (21), dereva bajaji na mkazi wa mtaa wa Bukala Wilaya ya Sengerema, kwa tuhuma za kutengeneza na kusambaza picha za mjongeo kwenye mitandao ya kijamii, ikiwemo TikTok, akitangaza kuuza mtoto wake kwa fedha kiasi cha milioni Tsh.1.6, kwa lengo la kutafuta umaarufu mtandaoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP. Wilbrod Mutafungwa, amesema ukamatwaji wa mtuhumiwa ulifanikishwa kutokana na taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Dodoma.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo, huku likitoa wito na onyo kali kwa wananchi kushirikiana katika kufichua matukio yanayohatarisha usalama wa watoto na kufedhehesha utu wa Mwanadamu na jamii kwa ujumla.