Mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wa Geita zimesababisha Wanafunzi saba wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Businda iliyopo Wilayani Bukombe Mkoani Geita kupoteza Maisha na 82 kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa Darasani.
Akizungumza kwa njia ya simu Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Paskas Muragili amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kusema miongoni mwa wanafunzi hao 82 wawili kati yao hali zao ni mbaya.
“Wakiwa darasani wakati mvua inanyesha ilipiga radi na saba wamepoteza maisha kwa muonekano sita ni wavulana na mmoja msichana lakini bado tunafuatilia kujua jinsi zao maana mimi sijaingia mochwari bado tunahangaika na hawa majeruhi” Mkuu wa wilaya ya Bukombe , Muragili.
Muragili amesema bada ya tukio hilo madaktari walifika haraka shuleni na wengine kupokea majeruhi hospitali na hadi sasa bado wanaendelea kuwahudumia majeruhi waliolazwa katika hospitali ya wilaya hiyo.