Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka Wilaya za Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma wamefanya matembezi maalum kuunga mkono azimio la chama hicho la kumpitisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais wa Tanzania na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, akiongoza matembezi hayo amesema uamuzi wa kuwapitisha viongozi hao ni sahihi kutokana na kazi kubwa waliyoifanya kwa Watanzania.
Amesisitiza kuwa maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia yanapaswa kuwapa wakazi wa Ruvuma sababu ya kujivunia na kuendelea kuiunga mkono CCM.
Aidha amewasihi pia wananchi wa mkoa huo kujikita zaidi kwenye shughuli za uzalishaji mali, hususan kilimo, kwani serikali imewekeza kwa kutoa pembejeo za ruzuku bure kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na kuleta tija.
Amewaagiza maafisa kilimo na ushirika kuhakikisha ugawaji wa pembejeo unafanyika kwa haki, bila upendeleo ili kila mkulima anufaike.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Simon Chacha, ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, zaidi ya Shilingi bilioni 300 zimetolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Miradi hiyo imehusisha sekta za maji, elimu, afya, umeme, barabara, mawasiliano, utawala bora, na huduma za kijamii.
Katika sekta ya elimu zaidi ya Shilingi bilioni 8 zilitumika kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa, maabara, mabweni, vyoo, na mifumo ya maji.
Sekta ya afya ilipokea Shilingi bilioni 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, nyumba za watumishi, na miundombinu ya maji na vyoo.
Kwa upande wa maendeleo ya kijamii na uchumi, zaidi ya Shilingi bilioni 11.3 zilitumika kwenye miradi ya TASAF, elimu bila malipo, ujenzi wa miundombinu ya shule kupitia mpango wa BOOST, na utoaji wa pembejeo za kilimo.
Sekta ya maji ilipokea Shilingi bilioni 8.2 kupitia RUWASA huku TARURA ikipokea Shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Namtumbo, Francis Mgoloka, amesema wilaya hiyo imepokea zaidi ya Shilingi bilioni 46.5 katika kipindi cha miaka minne, ambapo sekta ya elimu ilipata Shilingi bilioni 9, sekta ya afya Shilingi bilioni 3.3, umeme vijijini Shilingi bilioni 8, na sekta ya maji Shilingi bilioni 7.8.
CCM Mkoa wa Ruvuma imewahimiza wanachama wake kuendelea kueleza mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia ili wananchi waone namna serikali yao inavyoboresha maisha yao.
Pia, imewashukuru wananchi wa Tunduru kwa kuiamini CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita, ambapo chama hicho kilipata ushindi wa kishindo.