Maelfu ya Waumini wa Kanisa Katoliki wamekusanyika katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kumuaga Baba Mtakatifu Francisko.
Jeneza lake liliwekwa kanisani siku ya Jumatano, kufuatia matambiko ya awali yaliyofuatia kifo cha papa huyo Jumatatu asubuhi.
Waumini walilizunguka jeneza hilo huku baadhi yao wakipiga magoti kwa ishara ya heshima .
Miongoni mwa waliohudhuria ni wanandoa wapya, Luis na Macarena, ambao waliambia BBC kwamba walisafiri hadi Roma wakitarajia kupokea baraka za Papa Francis: “Papa Francis ni mtakatifu na atatubariki kutoka mbinguni,” Luis alisema.
Jeneza la Francis, ambalo litaendelea kuwa wazi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro hadi Ijumaa ijayo, lina baadhi ya alama tunazozieleza hapa chini.
01. VAZI JEKUNDU
Vazi mashuhuri zaidi ambalo huvaliwa na Papa Francis ni jekundu.
Ni vazi la kiliturujia linaloashiria upendo na huruma pamoja na damu iliyomwagika ya Kristo.
Aina hizi za mavazi huvaliwa katika tarehe muhimu katika mila ya Kikatoliki, kama vile Jumapili ya Mitende, Ijumaa Kuu, au siku ya Pentekoste.
02. KITAMBAA CHEUPE
Juu ya vazi jekundu papa amevalishwa kitambaa cheupe chenye msalaba uliopambwa na rangi nyeusi.
Ni pambo linalojumuisha kitambaa cha urefu wa mita mbili ambacho mapapa na maafisa wengine wa ngazi za juu huvaa mabegani mwao wakati wa misa ya papa.
Ni mapokeo kwamba vazi linalovaliwa na Papa limetengenezwa na watawa wa Kibenedikti wa Mtakatifu Cecilia huko Roma.
Juu ya paliamu pia kuna kipande cha dhahabu kinachowakilisha misumari ya Yesu Kristo, kipande ambacho kwa kawaida hujumuishwa katika mazishi ya papa.
03. JOHO JEUPE KICHWANI
Kichwani, Francis amevaa kilemba cheupe kilichopambwa kwa michirizi ya dhahabu.
Ni vazi refu na gumu ambalo huvaliwa na Papa na maaskofu katika hafla kuu na huwakilisha hadhi ya upapa, utakatifu na mamlaka.
Hapo awali, mapapa walivaa tiara, ambayo iliwekwa wakati wa ibada ya kutawazwa na katika matukio fulani maalum, kama vile baraka ya Urbi et Orbi. Papa Paul VI alikuwa wa mwisho kuivaa, mwaka 1963.
04. PETE YA FEDHA
Mwili wa Papa Francis umelazwa kwenye jeneza lake huku mikono yake ikiwa juu ya tumbo lake. Kwenye kidole cha pete cha mkono wake wa kulia, Papa amevaa pete ya fedha.
Hiki ni kipande ambacho Francis amekivaa tangu wakati wake kama askofu wa Buenos Aires.
Taratibu za kifo cha papa zinaonyesha kwamba Pete ya Wavuvi, ambayo papa huipokea anapochaguliwa kama ishara ya mamlaka ya upapa, lazima iharibiwe ili kuashiria mwisho wa mamlaka yake juu ya Kanisa Katoliki.
Mabaki hayo yanatumika tena kutengeneza pete ya Papa anayefuata. Lakini wakati Fransisko alipochukua madaraka kama papa wa 266, Papa Mstaafu Benedict XVI alikuwa hajafariki, hivyo pete mpya ilitengenezwa.
05. ROZARI (TASBIHI)
Papa Francis pia ana tasbihi mikononi mwake, kama mapapa wanavyofanya katika mazishi yao tangu Paulo VI.
Tasbihi ambayo Papa Francis anavalia ni ya busara, ikiwa na nyororo ya fedha, na msalaba mdogo.
Moja ya tofauti kubwa katika mazishi ya Papa Francis ni jeneza.
Majeneza yaliyotumika kwa maziko ya hapo awali ya papa yalikuwa ni majeneza matatu yaliyotengenezwa kwa miberoshi na madini ya risasi, lakini Francis aliomba azikwe kwenye jeneza la mbao na zinki.
Papa pia aliomba kubaki kwenye jeneza lililo wazi kwa ajili ya mazishi yake, huku mapapa wengine wakipumzishwa kwenye kwenye jukwaa linaloitwa catafalque.
Katika wosia wake, Fransisko aliomba azikwe katika kaburi lisilo na mapambo katika Kanisa Kuu la Kipapa la Mtakatifu Maria Meja wa Roma, tofauti na mapapa wengine waliozikwa katika kaburi la Vatikan la Basilica ya Mtakatifu Petro.
Chanzo BBC News Swahili