Ongezeko la taarifa za upotoshaji dhidi ya Serikali, limepelekea Viongozi, Chama cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu, kuzindua rasmi Kijani Fact Scan kwa lengo la kukabiliana na hali hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma, Katibu wa Idara ya Uhamadishaji na Chipukizi- UVCCM Taifa, Jesca Mshama amesema, upotoshaji huo unafanywa na baadhi ya Wanaharakati, Wanasiasa na watu kutoka Nje ya Nchi kwa makusudi ya kuchafua taswira ya Taifa, kuvuruga amani na mshikamano wa kijamii.
Amesema, “kupitia Kijani Fact Scan tutatoa taarifa sahihi na elimu kwa umma juu ya taarifa potofu zinazozunguka na njia ya kukabiliana nazo, tutajibu hoja kwa hoja kwa kutumia ushahidi, takwimu na tafsiri sahihi.”
“Tutahakikisha tunakataa propaganda chafu na kuziba mianya yote ya upotoshaji, tutamshirikisha kila kijana na kila mwanajamii Mzalendo, Kuwa sehemu ya ulinzi wa Taifa dhidi ya upotoshaji,” amesema Mshama.
Amesema Vijana Wakitanzania wamechoka chini ya Uongozi wa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Ali Kawaida wamechoka kuona jitihada za Serikali zikibezwa.
“Tumechoka kuona uongo ukipambwa kama hoja na kufanywa ukweli, tumechoka kuona amani ya Nchi ikitishiwa na propaganda”, amesema
“Kijana Fact Scan ni ajenda ya kila kijana, kila Mwanajamii Mzalendo aliyetayari kulinda Taifa lake dhidi ya uongo na upotoshaji”. Amesema Mshama