MENEJA wa TANESCO Wilaya ya Muheza Mhandisi African Chuwa amesema wizi wa nyaya za umeme kwenye maeneobtofauti wilayani humo ni tatizo mojawapo lililosababisha huduma ya umeme kutokuwa ya uhakika ndani ya wiki mbili zilizopita.
Mhandisi Chuwa ameyasema hayo ofisini kwake alipotembelewa na waandishi wa habari kufuatia malalamiko ya wananchi wilayani humo.
“Watu waliiba waya za kopa kwenye transformer 18 katika maeneo tofauti tofauti na kusababisha baadhi kufungua, wakati umeme ukizima ni lazima kutakuwa na majaribio ili kutambua eneo lenye tatizo”, amesema.
Amefafanua kwamba Wilaya hiyo inapelekea umeme katika Wilaya za Mjinga na Pangani, hivyo ili kubaini tatizo liko upande upi ni lazima kurejesha umeme na endapo ukizima tatizo linajulikana na kufuatiliwa.
“Kwahiyo huo wizi ulisababisha umeme kukatika mara kwa mara, hasa wakati huo wa kujaribisha kurudisha laini ili kujua tatizo lipo upande gani”, amefafanua Chuwa.
Sambamba na tukio hilo la wizi, amesema kuna matengenezo makubwa yanayofanyika katika kituo cha kuzalisha umeme cha Hale, ambayo yanapelekea kuzimwa kwa laini inayopelekea umeme wilayani humo.
Amesema katika kituo hicho kuna laini inayopelekea umeme Muheza lakini pia ipo inayopelekea umeme Wilaya ya Korogwe, hivyo wakati matengenezo yakiendelea kulikuwa na zoezi la kuzimwa kwa umeme katika laini hizo.
“Matengenezo haya ni miezi minne, hivyo bado yanaendelea mpaka mwezi wa nane, lakini pia kuna kituo kidogo cha kusambaza umeme pale Songa kuja Muheza kulikuwa na tatizo la kifaa cha kuzimia umeme, kwahiyo hizi wiki mbili, tatu, hizo ndiyo sababu kubwa za kukatika kwa umeme” amefafanua.
Hata hivyo Mhandisi Chuwa amesema kipindi hicho hakuna mwananchi yeyote aliyepeleka taarifa ya kupata madhara huku aliwataka kuwa wavumilivu katika kipindi ambacho matengenezo yataendelea.
Amebainisha kwamba matengenezo yanayoendelea kwasasa ni kukata miti iliyopo karibu na nguzo, kutoa nguzo chakavu na kuweka za zege ambazo haziozi lakini pia kwa maeneo ya milimani ambayo hayafikiki wanaweka nguzo za kawaida mpya.
“TANESCO haitaki kusikia kabisa kukatika kwa umeme, labda yatokee matatizo ya kuanguka kwa nguzo au wananchi wanaokata miti bila kutoa taarifa na kuanguka kwenye waya na sababu nyingine kama hizo,
“Kwahiyo tuwe wavumilivu kwasababu TANESCO tupo kazini tunapambana na tunatarajia mpaka huo mwezi wa nane tunaweza tukasema kwamba umeme hautakatika labda kutokee mambo ya kiasilia ambapo yapo nje ya uwezo wetu” amesema.