Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia kuhusu ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Benki hiyo, kikao ambacho kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.
Katika kikao hicho wamejadiliana kuhusu kuendeleza mageuzi ya kimfumo yanayolenga uthabiti wa kiuchumi, uboreshaji wa fedha za umma, uhimilivu wa deni la serikali, kukuza sekta binafsi katika ujumuishaji wa kijamii katika masuala ya kiuchumi na uangalizi wa mabadiliko ya tabianchi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Kamishna wa Idara Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, Kamishina wa Sera, Wizara ya Fedha, Dkt. Johnson Nyella, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Nuru Ndile na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na Benki ya Dunia.