
Leo asubuhi katika kazi, niliposhiriki katika harambee ya ujenzi wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Usonji cha Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kitakachojengwa Bagamoyo. Ninalipongeza Kanisa (KKKT) kwa kuamua kujenga kituo hiki kwa ajili ya malezi na makuzi ya watoto wetu. Hii ndiyo maana ya upendo na moja ya majukumu muhimu ya dini katika jamii yetu.
Katika kutambua, kutunga na kutekeleza sera zinazosaidia watoto wenye mahitaji maalum, Serikali imenunua vifaa tiba mbalimbali pamoja na kuwezesha uwepo wa wataalamu (wa lugha, elimu na tiba) kwa ajili yao. Kazi hii njema na sehemu ya jukumu la Serikali kwa wananchi inaendelea kuzaa matunda huku tukishirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo zile za dini.
Nimetumia pia wakati huu pamoja na watoto, viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwasihi viongozi wa dini na kila mwananchi kuhubiri amani, umoja, utulivu na kuliombea Taifa hasa tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.