
Wimbi jipya la maandamano linaloongozwa na kizazi cha vijana maarufu kama Gen Z nchini Kenya limeendelea kumweka Rais William Ruto katika hali ya wasiwasi, huku kauli maarufu ya waandamanaji “Ruto wantam” – ikiwa na maana ya kutaka rais huyo aongoze kwa muhula mmoja tu – ikisambaa mitaani.
Ruto alichaguliwa karibu miaka mitatu iliyopita kwa ahadi ya kuwalinda maskini na kukomesha ukatili wa polisi, lakini hali ngumu ya kiuchumi, madai ya rushwa na ukandamizaji wa raia vinaendelea kuchochea hasira za wananchi. Kwa sasa, kiongozi huyo anahisi ukali wa vijana waliotayari kuingia barabarani kupaza sauti zao.
Wachambuzi wanasema kuwa endapo Ruto anataka kupata muhula wa pili mwaka 2027, atalazimika kutimiza ahadi zake za kiuchumi na kuacha msimamo mkali. Badala yake, atahitaji kujenga maelewano zaidi na kizazi cha sasa cha vijana walioelimika na wanaotumia mitandao ya kijamii kwa ustadi mkubwa kushinikiza mabadiliko.
“Shida za kiuchumi na madai ya ukatili wa polisi vinaweza kuwa vizuizi vikubwa kwa matarajio ya Ruto ya kuchaguliwa tena,” alisema Mucahid Durmaz, mchambuzi wa masuala ya Afrika katika shirika la Verisk Maplecroft.
Katika maandamano ya hivi karibuni yaliyofanyika Jumatatu, watu 31 walithibitishwa kuuawa kote nchini, kulingana na ripoti ya shirika la haki za binadamu linaloendeshwa na serikali. Polisi walitumia risasi, gesi ya kutoa machozi na mizinga ya maji kuwatawanya waandamanaji.
Gen Z wapaza sauti: “Tunataka Rais atusikie”
“Nchi yetu haijatujali. Hatuwezi kulisha familia zetu. Tuko barabarani kuzuia kupanda kwa bei, kupinga utekaji nyara unaofanywa na polisi, na kutetea taifa letu,” alisema Festus Muiruri, kijana mwenye umri wa miaka 22 aliyekuwa akishiriki maandamano mjini Nairobi.
Lakini serikali ya Ruto imekuwa na mwitikio wa taratibu mno kwa matakwa ya umma. Mwaka jana, ilibidi afute mapendekezo ya kuongeza kodi baada ya waandamanaji kuvamia bunge kwa mara ya kwanza kabisa – tukio lililorushwa moja kwa moja kwenye runinga duniani kote.
Waziri wa mambo ya ndani, Kipchumba Murkomen, aliwataja waandamanaji wa Juni kama “magaidi” waliotaka kufanya “jaribio la mapinduzi.”
Tofauti na marais waliomtangulia, Ruto anakabiliwa na kizazi kipya cha vijana waliokomaa kisiasa, wanaotumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la harakati bila kutegemea wanasiasa wa upinzani.
Vijana hawa wa Gen Z, waliopata elimu ya bure tangu miaka ya 2000, hawana kumbukumbu ya utawala wa kiimla. Wengi wao walizaliwa baada ya Kenya kuingia mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Ripoti ya Afrobarometer inaonyesha kuwa kila mwaka, vijana takribani 800,000 wanaingia kwenye soko la ajira. Ingawa wengi wao wameelimika kuliko wazazi wao, bado hawana ajira, hali inayozidisha hali ya kukata tamaa.
Kifo cha bloga chazua moto
Hasira dhidi ya serikali ziliongezeka mwezi uliopita kufuatia kifo cha blogger Albert Ojwang akiwa mikononi mwa polisi. Tarehe 25 Juni, takribani watu 19 walikufa kwenye maandamano yaliyohusiana na kifo hicho.
Matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji yameanza kuwatisha wawekezaji katika uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki. Utafiti wa Stanbic Bank Kenya ulionesha kuwa matarajio ya wafanyabiashara yaliporomoka mwezi Mei hadi kiwango cha pili cha chini kabisa kuwahi kurekodiwa.
“Maandamano ya mara kwa mara na kufungwa kwa shughuli yataendelea kuathiri imani ya wawekezaji na kuzuia ukuaji wa kiuchumi, hasa kama serikali itaendelea kutumia nguvu badala ya mazungumzo,” alisema Jervin Naidoo wa shirika la Oxford Economics.
Licha ya hali hii, Bunge kubwa la chama tawala linalodhibitiwa na Ruto linamkinga dhidi ya tishio lolote la kung’olewa madarakani kwa sasa.
Aidha,upinzani umedhoofika na bado haujampata mgombea mwenye mvuto kwa uchaguzi wa 2027. Kwa kumuingiza Raila Odinga katika mazungumzo ya kitaifa mwaka jana, Ruto alifanikiwa kumdhibiti mpinzani wake mkuu.
