
Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema malengo ya kiukiritimba ya mataifa ya Magharibi na kutupilia mbali kwao wasiwasi wa kiusalama wa nchi yake ndivyo vilivyosababisha mzozo unaoendelea hivi sasa kati ya Moscow na Magharibi.
Putin amesisitiza kuwa, tofauti za kiidiolojia ni kisingizio tu kinachotumiwa kufanikisha maslahi ya kisiasa kwa nchi za Magharibi.
Ameongeza kuwa alitegemea kwamba kuanguka kwa Shirikisho la Urusi ya zamani USSR kungepunguza mvutano kati ya Urusi nan chi za Magharibi.”Pia nilifikiri kwamba mabishano makuu [kati yetu] yalikuwa ya kiitikadi,” ameeleza Putin na kuongezea kwa kusema: “pamoja na hayo, hata wakati Umoja wa Kisovieti ulipotoweka … mbinu ya kuyatoa maanani maslahi ya kimkakati ya Urusi iliendelea.”
Rais Putin ameendelea kueleza kwamba jitihada zake za kuwabainishia viongozi wa nchi za Magharibi wasiwasi wa Urusi ziliambulia patupu. “Magharibi waliamua kuwa hawahitaji kufuata sheria inapohusu Urusi, ambayo haina nguvu sawa na USSR.”
Amesisitiza kuwa kilichodhihirika ni kwamba, bila ya Urusi kujiweka katika nafasi ya kuwa taifa huru linalojitawala, halitazingatiwa na kuheshimiwa.
Moscow imetaja masuala kadhaa ikiwemo matashi liliyonayo shirika la kijeshi la NATO kwa Ukraine na usaidizi wa kijeshi wa Magharibi kwa nchi hiyo kuwa sababu kuu za mzozo wa kijeshi unaoendelea nchini Ukraine ambayo ilitaka isifungamane na upande wowote.
