
Familia ya marehemu Alute Mughwai Lissu imetangaza ratiba ya shughuli za kuuaga na kuzika mwili wa marehemu, ambapo ibada ya kuuaga itafanyika Jumatatu, Novemba 9, 2026, jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 3, 2026, msemaji wa familia, Vincent Lissu Mughwai, ambaye ni mdogo wa marehemu, amesema ibada hiyo itafanyika katika Kanisa la Mtakatifu Teresa kuanzia saa saba mchana.
Amesema baada ya ibada ya kuuaga, mwili wa marehemu utasafirishwa kuelekea mkoani Singida kwa ajili ya mazishi.
Kwa mujibu wa Vincent, mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumanne, Novemba 10, 2026, katika Kijiji cha Mahambe, ambacho ni nyumbani kwa marehemu na familia yake.
Katika hatua nyingine, Vincent amethibitisha kuwa ratiba ya familia kwenda mahakamani Ijumaa, Novemba 6, 2026, kusikiliza hukumu ya kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Antipas Lissu, haijabadilika.
Amesema familia itashiriki shughuli hiyo ya mahakamani kama ilivyopangwa kabla ya kuendelea na taratibu nyingine za kuuaga na mazishi ya marehemu.
Familia imeendelea na maandalizi ya kuhakikisha shughuli zote za kumuaga na kumzika marehemu zinafanyika kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa.
