
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Kigoma imekamilisha ujenzi wa barabara ya Bango-Burega-Ujiji yenye urefu wa Kilomita 7 kwa kiwango cha lami iliyotekelezwa chini ya mradi wa Uendelezaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) kupitia mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA wilaya ya Kigoma, Mhandisi Elias Mtapima ambapo amesema kuwa mradi huo umetekelezwa na kukamilika na wananchi wameanza kunufaika.
”Barabara hii imekuwa mkombozi kwa wananchi kwani mwanzoni ilikuwa inapitika kwa shida lakini sasa usafiri umekuwa nafuu hata bajaji zinafika na kurahisisha huduma ya usafiri”, amesema Mhandisi Mtapima.
Kuhusu ujenzi wa mitaro katika maeneo hayo, Mhandisi Mtapima ameeleza kuwa sambamba na kukamilika kwa barabara hiyo tayari wamekamilisha ujenzi wa mitaro inayosadia kupeleka maji moja kwa moja katika ziwa Tanganyika na kuondoa adha iliyokuwepo kwa wananchi.
Mmoja wa wanufaika wa Barabara hiyo, Bw. Mussa Wilson amesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kumepelekea maeneo yao kubadilika na kupanda thamani lakini pia maji hayawezi tena kutuama kwenye makazi ya watu kutokana na uwepo wa mitaro imara.
”Uzuri barabara hii hata ukiangalia unaona ni ya kiwango cha juu, tunaipongeza serikali kwa mradi huu na tunanufaika nao”, amesema Bw. Wilson.
Naye, Bw. Ramadhan Khamisi amesema kuwa ujio wa mradi huo si tu umependezesha maeneo yao bali umeondoa kero ya usafiri iliyokuwepo hasa kipindi cha masika.
