
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Novemba 18, 2026, anaanza ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini Uganda, kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Yoweri Kaguta Museveni.
Akiwa nchini Uganda, Rais Samia anatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Museveni, yatakayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa Tanzania na Uganda katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, mazungumzo hayo yanatarajiwa kujikita katika sekta za nishati, kilimo, viwanda, biashara na fedha.
Aidha, Rais Samia akiwa ameambatana na mwenyeji wake, anatarajiwa kutembelea na kuzindua kiwanda cha kuunganisha magari cha Double Q Automotive Assembly Plant kilichopo Wilaya ya Mpigi nchini Uganda.
Ziara hiyo inalenga kuendeleza ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Uganda pamoja na kupanua fursa za kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili.

