
Na Nyamiti A. Nyamiti
Jeshi la Polisi Wilaya ya Kahama limewataka wamiliki wa silaha wenye tabia ya kuzikodisha kwa watu na Makampuni ya Ulinzi kuacha mara moja kitendo hicho, kwani ni kinyume na matumizi halali ya silaha hizo na ni kosa kisheria.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kahama, S.S.P Maro Phortunatus Kenyunko, wakati wa hafla ya kutimiza miaka 10 ya Kampuni ya Ulinzi ya Dyanabo Security Group.

Kenyunko ameyataka Makampuni ya Ulinzi kufuata taratibu na masharti ya ulinzi yanayotolewa na Jeshi la Polisi nchini, kuzingatia stahiki za wafanyakazi na kujiepusha na tabia ya kuokoteza walinzi mitaani bila kufuata utaratibu.

Katika hatua nyingine, Kenyunko ameipongeza kampuni ya Dyanabo Security Group kwa kutimiza miaka 10 na kuzalisha ajira za Vijana 350, pamoja na kushirikiana vyema na Jeshi la Polisi Wilayani Kahama na nje ya mkoa katika kuimarisha ulinzi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Dyanabo Security Group na Mwenyekiti wa Makampuni ya Ulinzi Mkoa wa Shinyanga, Fabian Dyanabo, ametaja siri ya kampuni yake kuendelea kufanya vizuri ni pamoja na kuzingatia maslahi ya wafanyakazi na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa askari ili waweze kukabiliana na changamoto katika kazi zao.

Awali, akisoma risala kwenye hafla hiyo, Julitha Mlindwa, amesema dhamira ya kampuni hiyo ni kujenga kampuni yenye uwezo wa kutoa huduma za ulinzi zenye viwango vya kitaaluma, zinazoaminika na kukidhi mahitaji ya wateja.
Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo wamekiri kuwa kampuni imewasaidia katika kuendesha maisha yao baada ya kuajiriwa.

