
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, amesema kwa sasa hakuna mpango wa kuruhusu mapadre wa Kanisa hilo kufunga ndoa, licha ya kukiri kuwa suala hilo linaweza kubadilika katika siku zijazo.
Papa Leo XIV ameeleza kuwa suala la wanaume waliooa kuruhusiwa kuwa mapadre ni jambo lenye utata na linaweza kusababisha mgawanyiko ndani ya Kanisa Katoliki katika baadhi ya maeneo.
Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege ya Papa alipokuwa akirejea Vatican kutoka ziara ya siku 12 katika nchi za Amerika Kusini, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 71 alisema kipaumbele chake kwa sasa ni kuimarisha umoja na kuwaleta waumini pamoja.
Amesema ingawa kuna uwezekano wa baadhi ya mambo kubadilika siku zijazo, kwa sasa anaamini kuwa jukumu lake kubwa ni kuponya tofauti na kuimarisha mshikamano ndani ya Kanisa.
Kauli hiyo imekuja wakati mjadala kuhusu kuruhusu mapadre waliooa ukiendelea kwa miongo kadhaa, huku wanaounga mkono mabadiliko hayo wakidai kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza idadi ya wanaume wanaojiunga na huduma ya upadre na kusaidia kukabiliana na upungufu wa mapadre katika baadhi ya maeneo duniani.
Mjadala huo ulipata nguvu zaidi mwaka 2019 wakati mkutano wa maaskofu uliofanyika Vatican ulipomwomba aliyekuwa Papa Francis kuruhusu wanaume waliooa kupewa daraja la upadre katika maeneo ya mbali, hususan msitu wa Amazon, ambako kuna uhaba mkubwa wa mapadre.
Hata hivyo, Papa Francis, aliyefariki dunia Aprili 2025 baada ya kuliongoza Kanisa Katoliki kwa miaka 12, hakuchukua hatua ya kuruhusu mabadiliko hayo.
Kwa mujibu wa utaratibu wa Kanisa Katoliki, mapadre wengi hufuata kiapo cha useja, kinachowataka kuishi bila kuoa au kuolewa.
Katika ziara yake ya hivi karibuni, Papa Leo XIV alitembelea Uruguay na Argentina kabla ya kuhitimisha safari yake nchini Peru, ambako aliishi kwa takribani miaka 20 na pia ana uraia wa nchi hiyo.
Papa huyo pia alizungumzia tukio la mtu aliyemtupia rozari wakati akiwasalimia waumini kupitia gari maalumu la Papa, ambapo rozari hiyo ilimpiga kwenye jicho.
Akilizungumzia tukio hilo, alieleza kuwa linaonesha namna waumini wa Peru walivyo na imani kubwa na shauku ya kupokea baraka za Kanisa.
