
ARUSHA: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili jijini Arusha leo Novemba 19, 2026, akitokea nchini Uganda alikokuwa akifanya ziara ya kikazi ya siku mbili.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea katika eneo la Ngaramtoni, Rais Samia amewahimiza wakazi wa Arusha kutumia fursa zitakazotokana na mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini mwaka 2027.

Rais Samia amewataka wamiliki wa hoteli na wafanyabiashara kuongeza uwekezaji katika huduma za malazi na biashara mbalimbali ili kujiandaa kupokea wageni watakaotembelea nchi wakati wa mashindano hayo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kukamilisha miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wageni wanapata huduma muhimu wanapowasili jijini Arusha, huku akiwataka wananchi kudumisha usafi, amani na utulivu.
“Tukiwa salama, wageni wetu watakuja, watacheza na kuondoka salama,” amesema Rais Samia.
Katika hatua nyingine, akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Arumeru, Rais Samia amesema Serikali imetenga Shilingi bilioni 500 kwa ajili ya uendelezaji wa miradi ya maji mkoani Arusha, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo.
Rais Samia anaendelea na shughuli zake jijini Arusha, ambapo kesho Novemba 20, 2026, anatarajiwa kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi utakaofanyika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Vilevile, Novemba 21, 2026, anatarajiwa kutunuku kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Chuo cha Kijeshi Monduli, mkoani Arusha.

