Na Evelyne Ernest – Kagera
SIKU chache baada ya Ofisi ya Udhibiti wa Taka na Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, kusema kwamba suala la kuzoa taka wakati wa usiku katika dampo la Soko Kuu la Manispaa hiyo, haliwezekani kutokana na miundombinu iliyopo, Naibu Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Steven Byabato, ameahidi kushughulikia tatizo hilo na kuhakikisha linafanyika, ili kuwasaidia wananchi kuondokana na adha zinazotokana na uzoaji wa taka hizo mchana.
Naibu Waziri Byabato, ameyafafanua hayo wakati akizungumza na Divine FM, akisema awali suala la kuzoa taka wakati wa usiku lilikuwa limetekelezwa na kuonekana kushangazwa kwa nini lilisimamishwa, ambapo ameahidi kulifuatilia na kulisimamia kwani kama Ofisi hiyo inavyodai kuwa mazingira ya eneo la Buhembe zinakotupwa taka hizo ni magumu na hatari kwa wazoaji kutokana na kutokuwepo kwa taa, linaweza kufanyiwa kazi kwa kuweka taa kwenye eneo hilo ili kuwaondolea adha wananchi wanaokumbana na changamoto za kiafya pindi taka za dampo hilo zinapozolewa mchana.
Hata hivyo Kiongozi huyo amekiri kuwepo kwa changamoto kubwa ya taka ambazo zinazidi kiwango kwenye maeneo ya Manispaa ya Bukoba, hivyo kueleza kwamba katika fedha zinazoombwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kadhalika suala hilo litaingizwa ili ipatikane fedha ya kununua magari mazuri ya kubebea taka, ambayo yanaweza kufanya kazi hiyo hata wakati wa mchana bila kuleta adha yoyote kwa wananchi.
Naye Diwani wa Kata ya Bilele lilipo Soko hilo Tawfiq Sharifu, amesema amesubiri kuliwasilisha suala hilo kwenye kikao cha Kamati na Baraza la Mwezi Julai Mwaka huu, ili kuuliza utekelezaji wake, kwani hivi karibuni baada ya kufanya mkutano wa wafanyabiashara na kuomba taka zizolewe usiku kutokana na adha iliyopo wakati wa mchana ikiwamo harufu mbaya na kuzuia vyombo vya usafiri, walikubaliana kufanya hivyo na kama haiwezekani ni vyema ikatafutwa Kampuni itakayoweza kuzoa taka hizo kwani tayari Kata ya Hamgembe wameanza kuweka vikundi vya uzoaji taka ili kuondoa adha za namna hiyo, hivyo kutumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuwa wavumilivu wakati suala hilo likiendelea kupitishwa kwenye mchakato wa utekelezaji.